Mkaguzi wa TBS akitoa bidhaa ambazo hazina muda wa matumizi
Bidhaa zilizoisha muda wake
Bidhaa zenye viambata sumu ambazo zimepigwa marufuku.
*************************************************
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kufanya ukaguzi ukiendana na kutoa elimu kuhusiana na makundi 13 ya bidhaa za vipodozi kutokana na watu wengi kukumbana na changamoto ya kutambua nini maana ya bidhaa za vipodozi.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa shirika hilo wa kufanya ukaguzi unaoendana na kutoa elimu kuhusiana na vipodozi kwa wananchi katika wilaya zote za mikoa ya kanda ya ziwa na tayari ukaguzi na elimu imetolewa kwenye Wilaya za Nyamagana na Ilemela, jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa bidhaa za vipodozi uliofanywa
na Ofisi ya TBS Kanda ya Ziwa, Kaimu Mkuu wa Kanda hiyo, Evarist Mrema, alisema ukaguzi huo ukiendana na kutoa elimu unafanyika kwenye maduka ya rejareja, jumla, kwa wasambazaji, supermarkets, migahawa na kwingineko.
Akifafanua zaidi, Mrema alisema; ” Tunafanya ukaguzi na kutoa elimu kwa upande wa vipodozi, kwani watu wamepata changamoto ya kujua ni nini maana ya bidhaa za vipodozi, tunaliona hilo nalo ni changamoto kwenye ukaguzi huu na tunahitajika kutoa elimu na tunatoa elimu na tunaendelea kutoa elimu wakati wa ukaguzi.”
Alisema aina za vipodozi zipo katika makundi 13 na kundi la kwanza ni za bidhaa za watoto kama vile poda, shampuu na kundi la pili ni la bidhaa zinazotumika bafuni.
“Huko nako kuna bidhaa tofauti zinazotumika bafuni kama sabuni za
kuogea pamoja na zile ambazo watu wanaziandaa katika maeneo yao ya
kuogelea na vitu kama hivyo,” alisema Mrema.
Alitaja kundi lingine kuwa bidhaa za nywele ambako kuna makundi yake
kama mawili au matatu. Kwa mujibu wa Mrema kuna rangi za nywele ambazo
zinatumika kwenye nywele, lakini pia kuna nywele zinazoongezwa ndani
ya nywele asili kama rasta na wigi na kwamba hizo zote ni aina za bidhaa za vipodozi.
Bidhaa nyingine kwa mujibu wa Mrema ni zile ambazo zinapakwa juu ya
ngozi kama mafuta ya kupaka, losheni na bidhaa nyingine zinatumika kwa
upande vidole vya akina mama mfano kucha bandia na midomo ambazo nazo ni sehemu ya bidhaa za vipodozi.
Alitaja aina nyingine za bidhaa za vipodozi kwa upande wa urembo
zinazotumika kwenye macho akisema zote hizo ni aina za vipodozi na
wananchi wataendelea kufamua kaguzi zinazoendana na kutoa elimu kuhusiana na bidhaa hizo.
Wakizungumzia kuhusiana na ukaguzi huo, wananchi wengi walielezea kufurahishwa na hatua hiyo kwani wamekuwa wakibambikwa bidhaa za chakula na vipodozi zilizokwisha muda na vilevile kuuziwa vipodozi zenye viambata sumu.
“Kwa hiyo shirika linatusaidia kuwadhibiti na waendelee kwa nguvu hiyo hiyo hadi maduka ya vijijini,” alisema mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Machibya Samuel.
Wauzaji madukani wameomba shirika liwafikirie katika malipo ili walipe kwa mikupuo miwili au zaidi kama wanavyofanya TRA, kwani biashara ni ngumu.