Ng’ombe wakiwa katika Hifadhi ya Wanyamapori ya Isawima wilayani Kaliua kama walivyokutwa jana na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati (mbele mwenye suti nyeusi) akiangalia jana uharibifu wa ukataji miti ovyo uliofanywa na wavamizi wa msitu wa hifadhi ya wanyamapori wa Isawima wilayani Kaliua
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Abel Busalama (kulia) akimweleza jana Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati(wa pili kutoka kulia) na wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Mkoa jinsi makundi mbalimbali yanayovamia eneo hilo na kuharibu mapito ya manyama kama vile Tembo.
MKuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati (mbele mwenye suti nyeusi) akitoa maelekezo jana kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuwaondoa wavamizi wa msitu wa hifadhi ya wanyamapori wa Isawima wilayani Kaliua
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Abel Busalama (kushoto) akimweleza jana Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati(kulia) jinsi makundi mbalimbali yanayovamia eneo la Hifadhi ya Msitu wa Wanyamapori la Isawima wilayani Kaliua na kuendesha shughuli za kibinadamu zinazotishia uendelevu wake.
************************************************
NA TIGANYA VINCENT
HATIMAYE Serikali imekabidhi usimamizi wa eneo la Hifadhi ya Wanyamapori ya Isawima lilipo wilayani Kaliua kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ili kukomesha uharibifu maliasili ikiwemo ukataji magogo na uwindaji haramu wa wanyamapori unaofanyika katika eneo hilo.
Hatua hiyo inafuatia Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Isawima kushindwa kudhibiti vitendo vya uharibifu na mauaji ambayo yanaendelea ndani ya Hifadhi hiyo.
Makabidhiano ya awali yamefanywa jana na Mkuu na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwapa TAWA ili waweze kuanza kazi ya kulinda Hifadhi hiyo.
Alisema Serikali imechukua hatua hiyo baada ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Isawima kutokamilisha taratibu za usajili na kutokuwa na uwezo na nguvu za Kisheria za kuisimamia hifadhi hiyo hali iliyopelekea kuendelea kwa ujangili, mauaji na kusababisha tishio kubwa la kutowekwa kwa Hifadhi hiyo.
Dkt. Sengati alisema Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Isawima haina rasilimali za kutosha kukabiliana na uharibifu katika eneo hilo na hivyo kufanya kuwepo kwa makundi ya wavamizi ndani ya mistu.
Alisema kufuataia kukosekana kwa rasilimali vitu na watu wamekuwa wakingonja uharibifu utokee ndio waende kwa ajili ya kujipatia fedha toka kwa waharifu zinazotokana na uuzaji wa magogo na faini ,badala ya kufanya kazi ya kuzuia uharibifu kwa ajili ya uendelevu wa maliasili hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Dkt. Sengati alisema mtindo huo wa usimamizi umesababisha kuzuka kwa migogoro ya mara kwa mara ambayo kwa upande mwingine imesababisha hata watu kupoteza maisha.
Aliwataka TAWA baada ya kupewa jukumu hilo ,kufanyakazi kwa uzalendo katika kulinda rasilimali hiyo muhimu kwa wakazi wa mikoa ya Tabora na Kigoma ili Serikali isije ikaona kuwa imekosea kuwapa jukumu la usimamizi.
Dkt. Sengati aliongeza kuwa katika usimamizi ni vema wakaendelea kushirikiana na vijiji vilivyotoa ardhi yao kwa ajili ya uanzishaji wa Hifadhi hiyo ili nao waone manufaa ya kuwepo kwake.
Alisema wanaweza kuwashirikisha kwa kuwaruhusu kufanya shughuli ambazo haziathiri uhifadhi kama vile ufugaji wa nyuki katika eneo la Hifadhi na kutoa michango kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo kama vile kuwajengea shule na Zahanati sehemu ambazo hawana.
Dkt. Sengati aliwataka kufanyakazi katika kuhakikisha wavamizi wote na vikundi vyote vya uhalifu vilivyomo ndani ya msitu huo vinaondoka ili uharibifu usiendelee.
Alisema lengo la Serikali ni kutaka msitu huo hatimaye uje upande kwa ajili ya kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua na Taifa kwa ujumla.