Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani kuhusiana na mikakati ambayo wameiweka katika kuborsha hali ya usafi wa mazingira pamoja na kuweka mpango kazi katika suala zima la kuleta maendeleo.
……………………………………………………………..
NA VICTOR MASANGU, BAGAMOYO
Mkuu wa Wilya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa amewaonya vikali baadhi ya dereva , makondakta pamoja na wananchi wenye tabia ya kutupa taka ovyo katika eneo la stendi ya mabasi madogo na maeneo mengine kwani kufanya hivyo kunasababisha uchafuzi wa mazingira na kunaweza kupelekea kuleta madhara makubwa ya kuibuka kwa mlipuko wa magonjwa mbali mbali ikiwemo kipindupindu.
Kawawa aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na changamoto za usafi wa mazingira katika baadhi ya maeeno pamoja na mipango endelevu waliyojiwekea katika kuthibiti hali ya mlipuko wa magonjwa mbali mbali pamoja na kuhakikisha kwamba sehemu zote zinakuwa katika hali ya usafi katika kipindi chote na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kupigwa faini na kupelekwa mahakamani.
“Kitu kikubwa ambacho ninawaasa baadhi ya madereva ambao wamekuwa wakivunja taratibu ambazo tumeziweka katika kuhakikisha kwamba suala la usafi wa mazingira linazingatiwa kwa kiasi kikubwa hivyo nimarufuku kabisa kutupa takataka ovyo katika eneo la stendi yetu pamoja na maeneo mengine hii ni kwa ajii ya manufaa ya wananchi wote wa Wilaya ya bagamoyo na kama unavyojua sasa hivi tuna halmashauri mbli na tayari madiwani wameshaweka mikakati katika jambo hili la usafi katika maeneo tofauti,”alisema Kawawa.
Pia katika hatua nyingine aliongeza kuwa madereva hao kwa sasa wanapaswa kubadilika kwa kufanya usafi katika sare zao ambazo wanakuwa wakizitumia ili waweze kuwa safi na kwamba wahakikishe wanaweka utaratibu mzuri katika gari zao la kuwa na sehemu au kifaa kwa ajili ya kuweza kuwapa fura abiria waweze kuhifadhi takataka pindi wanapokuwa katika safari.
“Mara nyingine unaweza kukuta abiria wengine wananunua vitu njiani kwa ajili ya kuweza kula lakini sasa kutokana na gari husika kutokuwa na sehemu ya kutupia taka wanaamua kutupia dirishani hii nayo ni changamoto kubwa na pia inafanya mazingira kuonekana machafu na kwa hali hiyo ni hatari sana kwa usalama wa afya za wananchi hasa katika kipindi cha mvua zinaponyesha,”aliongezea Kawawa.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo aliwawakumbusha wananchi wa Bagamoyo kwa ujumla kuendelea kutimiza Agizo la Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu la kufanya usafi katika maeneo mbali mbali kila jumamosi ya mwisho wa mwezi ili kuboresha zaidi mazingira na kuthibiti mlipuko wa magonjwa ambayo yanaweza kujitiokeza kutokana na kukithiri kwa uchafu.