Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari.
………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, inamshikilia Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Kimotorok, Merubo Parimelo na mjumbe mstaafu wa Serikali ya Kijiji hicho Daniel Melau.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu amesema watuhumiwa hao wanashikiliwa kwa tuhuma za mbalimbali ikiwemo kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Makungu amesema watuhumiwa hao walipopekuliwa wamekutwa na nyaraka za Serikali.
Amedai kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakizitumia nyaraka kuuza ardhi ya kijiji kwa kurudisha tarehe nyuma ili kuonyesha mauzo hayo yalifanyika wakingali madarakani.
“Uchunguzi zaidi umeonyesha kuwa baadhi ya wenyeviti wastaafu wa vijiji katika Wilaya ya Simanjiro huondoka na nyaraka za vijiji kwa nia ya kutenda uhalifu wa kuuza ardhi japo wameshaondoka madarakani,” amesema.
Amewataka wote walioondoka na nyaraka wazirejeshe mara moja na kuzikabidhi kwa maofisa watendaji wa vijiji wanaohusika.
“Wasiporejesha wafahamu kuwa watakutana na mkono wa sheria kama wenzao kina Parimelo na Melau,” amesema Makungu.
Amewataka wafahamu kuwa Serikali ina mkono mrefu hivyo itaendelea kuwafuatilia.