Waziri wa Mifugo na uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ametoa zuio kwa wananchi wa kanda ya ziwa kula nyama ya nguruwe ikiwa katika kukabiliana na mlipuko wa homa ya nguruwe uliotokea hivi karibuni baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Shinyanga.
Waziri Ndaki ametoa zuio hilo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema taarifa zilizopo zinaonyesha homa ya nguruwe ilianzia kwenye halmashauri 6 za kanda ya ziwa.
“Kutokana na uwepo wa homa ya nguruwe tumewataka wananchi wa kanda ya ziwa kuacha kula nyama ya nguruwe ilikukabiliana na ugonjwa huu hatari ambao hauna tiba wala kinga wakati wataalamu wetu wanatafuta suluhisho” amesema Ndaki.
Amewaagiza wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanasimamia kikamilifu karantini zilizowekwa kwaajili ya kutibu nguruwe ambao tayari wameathirika na ugonjwa huo.
“Nawaagiza viongozi mnaohusika mikoani na wilayani kuhakikisha mnasiamia karantini zilizowekwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa ugonjwa huu hausambai kwenda maeneo mengine na kuleta madhara” amesema
Waziri Ndaki amezitaja halmashauri ambazo hazitaruhusiwa kula nyama ya nguruwe kuwa ni pamoja na Mbogwe,Sengerema,Geita,Misungwi,Kyerwa na kahama ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathilika na ugonjwa huo.
Amebainisha kuwa mpaka kufikia januari 22 mwaka huu zaidi ya nguruwe 1500 sawa na asilimia 10 ya nguruwe wote nchini wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Ameongeza kuwa “Serikali inaendelea kufuatilia na kufanya kila linalowezekana kuhakikisha ugonjwa huu unadhibitiwa haraka iwezekanavyo iliusienee katika maeneo mengine na kusababisha hasara kwa wafugaji wengi zaidi” alieleza
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Magonjwa ya Mifugo nchini Dkt Ezron Nonga amesema lengo la kuzuia wananchi kula nyama ya nguruwe ni kudhibiti ugonjwa huo usienee kwa kasi katika maeneo mengine ambayo bado.
Amewataka wafugaji wahakikishe wanatoa taarifa za ugonjwa au vifo vya nguruwe Mara vinapotokea, na pindi wanapokufa kuhakikisha wanazikwa kwa kuchimba shimo refu au kuteketezwa kwa moto
“Ugonjwa wa homa ya nguruwe huanzia kwa nguruwe pori na baadaye husambaa kwa nguruwe wa kufugwa kwa njia ya kugusana,damu,mate,kinyesi na maji maji mengine yanayotoka kwa wanyama wagonjwa au kugusa vifaa vyenye maambukizi” amesema Nonga