Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo anasikitika kutangaza kifo cha Afisa Mkuu Brigedia Jenerali Emmanuel Edward Maganga (Mstaafu), kilichotokea usiku wa tarehe 21 Januari, 2021 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Jeshi ya Kanda, Milambo Mkoani Tabora.
Marehemu Brigedia Jenerali Emmanuel Edward Maganga (Mstaafu) alizaliwa tarehe 18 Aprili, 1955 katika Kijiji cha Mombo, Kata ya Mombo, Tarafa ya Mombo, Wilaya ya Korogwe, katika Mkoa wa Tanga. Alipata Elimu katika ngazi mbalimbali ikiwemo Stashahada ya Uandishi wa Habari (Diploma in Journalism) kutoka Chuo cha Nyegezi Mwanza sasa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania.
Marehemu alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tarehe 01 Januari, 1979. Alihudhuria kozi ya Afisa Mwanafunzi nchini Tanzania na kutunukiwa Kamisheni tarehe 03 Aprili, 1980. Marehemu alipandishwa cheo kuwa Brigedia Jenerali tarehe 02 Septemba, 2011 kulingana na kozi za Kijeshi alizohudhuria katika utumishi wake. Marehemu alitumikia Jeshi kwa muda wa miaka 37 na mwezi 1 hadi alipostaafu utumishi Jeshini kwa umri tarehe 31 Januari, 2016.
Marehemu Brigedia Jenerali Maganga (Mstaafu) alitunukiwa Medali mbalimbali wakati wa utumishi wake ifuatavyo:- Miaka 20 ya JWTZ; Utumishi Mrefu Tanzania; Miaka 40 ya JWTZ; Utumishi Uliotukuka Tanzania; Miaka 50 ya JWTZ; Miaka 50 ya Muungano; Miaka 50 ya Uhuru na Nishani ya Comoro.
Katika Utumishi wake Jeshini, aliwahi kushika madaraka mbalimbali yakiwemo, Afisa Mnadhimu Makao Makuu ya Jeshi; Kaimu Mkurugenzi, Tawi la Usalama na Utambuzi, Makao Makuu ya Jeshi; Mwambata Jeshi nchini Marekani; Mkuu wa Ukaguzi Jeshini, Makao Makuu ya Jeshi; Madaraka aliyohudumu hadi anastaafu tarehe 31 Januari, 2016; Rais na Amiri Jeshi Mkuu alimteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma (Baada ya Kustaafu), tarehe 13 Machi, 2016 hadi tarehe 03 Julai, 2020.
Heshima za mwisho kwa marehemu zitatolewa nyumbani kwa marehemu Yombo Buzza Dar es Salaam tarehe 24 Januari, 2021 Kuanzia saa 2:00 asubuhi. Baada ya hapo Mwili wa marehemu utasafirishwa kwenda Turiani Mkoani Morogoro kwa mazishi yatakayofanyika Jumatatu tarehe 25 Januari, 2021.