Mkuu wa mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti aliyeshika mkasi akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa barabara iliyopewa jina la Mujungi iliyojengwa kwa kiwango cha lami ikiwa na urefu wa km 19 kutoka Mueba mjini hadi Rubya.
Mkuu wa mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti mwenye nguo za kijeshi akisoma jiwe la uzinduzi wa barabara ya Mujungi yenye urefu wa km 19 iliyojengwa kwa kiwango cha lami kutoka Muleba Mjini hadi Hospital ya Rubya.
Familia ya Marehemu Mhandisi Leopold Mujungi, Mkuu wa mkoa Kagera Mkuu wa mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti mwenye nguo za kijeshi pamoja na viongozi mbalimbali wakiomba sala na dua kwenye makabuli ambako alilazwa Mhandisi Leopold Mujungi aliyekuwa mkurugenzi wa barabara kuu Tanzania Bara.
…………………………………………………………………………..
Na Allawi Kaboyo – Mueba.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti ametekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli la kuzindua barabara yenye urefu wa kilomita 19 iliyojengwa kwa kiwango cha lami ambayo aliagiza ipewe jina la mhandisi Leopold Mujungi.
Agizo hilo la kuzindua na kuipa jina barabara hiyo, limetekelezwa januari 21,mwaka huu ikiwa ni baada ya siku tano tangu kutolewa kwake na Rais Magufuli aliyeagiza barabara hiyo izinduliwe na kuitwa jina la Mujungi, kutokana na kufanya kazi kwa uadilifu na kutoa mchango mkubwa kwa taifa.
Akizungumza wakati wa kukamilisha itifaki hiyo ya uzinduzi wa barabara hiyo, Gaguti amewataka watumishi wenzake wa umma kufanya kazi kwa uadilifu na kuweka maslahi ya taifa mbele huku akimshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa miradi mbalimbali inayotekelezwa mkoani Kagera.
“Leopold Mujungi ni marehemu lakini bado anapata heshima kwa utumishi wake uliotukuka na kwa uzalendo wake, hili ni somo kubwa kwetu, tufanye kazi kwa uadilifu mkubwa, tusitegemee malipo ya ziada, tuweke maslahi ya taifa mbele, malipo mengine tunaweza kuyapata hata tukishakufa maana waliobaki watakuwa wakitambua utendaji wetu” amesema.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo meneja wa wakala wa barabara nchini – TANROADS mkoa wa Kagera mhandisi Andrea Kasamwa amesema kuwa barabara hiyo imejengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni saba na kuongeza kuwa ilikamilika tangu mwezi desemba mwaka jana.
Sanjali na hayo Mkuu huyo wa mkoa akiambatana na viongozi wengine wamefika nyumbani kwa familia ya Leopold Mujungi na kumuomba mama kuhamia kwenye nyumba ambayo Rais Magufuli aliagiza ijengwe kwaajili ya heshima ya Mhandisi Mujungi kwa kuwa nyumba hiyo imekamilika.
Aidha viongozi hao wameweza kufika kwenye makaburi ya familia hiyo ambapo pia alizikwa mhandisi Mujungi na kumuombea sala na dua ili mwenyezimungu aweze kumpumzisha kwa amani.