………………………………………………………………………………
Na Alex Sonna, DODOMA
SERIKALI imetumia Sh.Bilioni 16.4 kukarabati miundombinu ya shule za ufundi za sekondari zilizopo kwenye mikoa tisa nchini.
Kufuatia uboreshaji huo, Wakuu wa Mikoa tisa wametakiwa kuhakikisha wanakuwa walezi wa shule hizo ili zitoe vijana wenye umahiri wa kutosha na wabobezi kwenye vitu mbalimbali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo, ametoa agizo hilo leo Januari 22,2021 alipokuwa akizungumza na Wakuu hao kwa njia ya ‘video conference’, Jijini Dodoma.
Amefafanua kuwa Shule sekondari ya ufundi ya Bwiru ilipewa Sh.Milioni 825, Chato Sh.Bilioni 3.9, Ifunda Sh.Bilioni 3.6, Iyunga Sh.Bilioni 1.01, Moshi Sh.Bilioni 2.1, Mtwara Sh.Bilioni 1.3, Musoma Sh.Bilioni 1.2, Mwadui Sh.Milioni 226 na Tanga Sh.Bilioni 2.1.
Waziri Jafo amesema kuwa wakuu hao wa mikoa wenye shule hizo wanapaswa kuzitembelea na kuzungumza na walimu ikiwa ni pamoja na waajiriwa wapya ili kueleza kwa mapana mikakati ya serikali ya kuinua ubora wa shule hizo.
Aidha, amesema jumla ya Sh.Milioni 30 zimetengwa kwa Kila shule kwa ajili ya ununuzi wa mitambo na vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika shule zote hizo za ufundi za sekondari za serikali.
“Baada ya Rais John Magufuli kutangaza na kutoa dira ya kuelekea uchumi wa viwanda mwaka 2016, Ofisi ya Rais Tamisemi ilichukua hatua mbalimbali ili kufanya maandalizi ya wataalamu ambao baadae watatumika katika viwanda vinavyoendelea kujengwa nchini,”amesema.
Amesema wataalamu hao watatoka katika shule hizo za sekondari za ufundi ambapo hatua zimechukuliwa ili kuimarisha utoaji wa elimu ya ufundi na kuifanya iendane na mahitaji na ushindani katika ulimwengu wa ajira ili kuongeza pato la mwananchi wa taifa kwa ujumla.
Amesema ili kuhakikisha ufundishaji na ujifunzaji katika shule hizo Novemba mwaka 2020, Serikali iliajiri walimu 150 wa masomo ya ufundi wa fani mbalimbali kwa wastani wa walimu 16.
Ametoa wito kwa wakurugenzi watendaji wa Halmshauri wenye shule hizo kuhakikisha miundombinu na vifaa vinatunzwa.