***********************************************
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Katika kutekeleza kauli mbiu ya Mkuu wa Mkoa Mtwara Mhe. Gelasius Gasper Byakanwa ya “Ondoa mapori, ongeza uzalishaji” Tarafa ya Mihambwe imeshiriki mafunzo ya kuondoa mikorosho isiyozaa na namna ya upandikizaji wa Mikorosho mipya yaliyofanyika leo Ijumaa Januari 22, 2021.
Mafunzo hayo kwa nadharia na vitendo yameongozwa na ofisi ya kilimo wilaya kwa uratibu wa ofisi ya Tarafa Mihambwe ambapo Maafisa ugani pamoja na Wananchi wamefundishwa namna gani ya ukataji miti isiyozaa na upandikizaji wa miti mipya ya Mikorosho.
Mkulima Mzee Juma Abdallah Chihuka aliishukuru Serikali kuja na mkakati huu wa kuongeza uzalishaji ambao utakuwa mkombozi wa kiuchumi kwao.
“Kwa muda mrefu nilikuwa nahitaji elimu hii, naishukuru sana Serikali ya Rais Magufuli kuingilia kati na sasa tunatarajia uzalishaji kuongeza kwani Mimi na wenzangu nipo tayari kwa maelekezo na ufanyaji kazi ilimradi uzalishaji uimarike kama awali.” Alisema Mzee Chihuka akiwa shambani kwake kitongoji cha Shangani kata ya Mihambwe.
Naye Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu amewasihi Wananchi kote kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata maelekezo ya Wataalamu wa kilimo ili kuokoa zao la Korosho kwani Serikali ipo pamoja nao kuwapa msaada wa hali na mali.
“Kwanza niwapongeze ofisi ya kilimo wilaya kwa kuamua kutoka ofisini na kuja shambani kutoa elimu ya uzalishaji bora wa zao la Korosho. Pili, kwa Wananchi waendelee kushikamana na Serikali na kutii maelekezo ya viongozi wa Serikali na Wataalamu wa kilimo kwani Serikali ipo kwa ajili yao, jukumu lao kubwa ni kufanya kazi kama ambavyo tunavyowasisitiza kila siku na ndani ya muda mfupi wataona matokeo makubwa ya uzalishaji kuongezeka.” alisisitiza Gavana Shilatu.
Katika ziara hiyo ya mafunzo Gavana Shilatu aliambatana pamoja na timu ya Wataalamu wa Kilimo toka wilayani, Maafisa ugani wa kata na vijiji, Watendaji kata na wakataji ambao walishiriki elimu ya nadharia iliyofanyika ofisi ya Mtendaji kata Mihambwe na baadae elimu ya vitendo iliyofanyika shambani ikihusisha Wananchi kwa ujumla.