***********************************************
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli, wilayani Lushoto Mkoani Tanga, January Makamba amemwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwasaidia wakulima wa chai wa jimbo hilo kumaliza tatizo la kuendelea kusimama kwa kiwanda cha chai cha Mponde.
January Makamba alitoa ombi hilo katika kikao cha Wadau wa Zao la Mkonge kilichofanyika jijini Tanga na kuongozwa na Waziri Mkuu.
Alisema kuwa wakulima wa zao hilo wa chai walifarijika sana wakati Waziri Mkuu alipofanya ziara mahususi kwa ajili ya kutatua mgogoro huo na walifarijika pia walisikia ahadi za serikali kufungua kiwanda hicho.
Makamba alimwomba Waziri Mkuu asaidie ili kufikia tamati ya tatizo kama ilivyotolewa ahadi na serikali.
Alishauri kuwa kama kuna changamoto zinazozuia uharakishaji wa kufungua kiwanda basi serikali ichukue hatua ya kukaribisha wawekezaji kwa kutangaza tenda ya kuendesha kiwanda hicho.
Akijibu ombi hilo, Waziri Mkuu alimhakikishia Mbunge na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, Amiri Shehiza kuwa serikali inafuatilia kwa karibu tatizo hilo ili wakulima waweze kuchakata majani maichi ya chai karibu na mashamba yao.
Majaliwa alieleza kuwa serikali ilikuwa na mazungumzo kujua namna bora ya kufufua kiwanda hicho na akaendelea kuwa serikali imefanya ukaguzi na imeridhia ripoti hiyo.
“Tumezungumza na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) tumeshauri wawatumie wataalamu wazee wazoefu ili waanze kuwashawasha mitambo wajue wapi kuna matatizo ili yarekebishwe,” alieleza
Alisisitiza kuwa nia na malengo ya serikali ya awamu ya tano kuona wakulima wa chai wa Bumbuli wanachakata majani ya chai karibu na mashamba yao.
Wakulima kwa sasa wanalazimika kukata majani hayo na kuyasafirisha hadi kiwanda cha Hekulu ambacho hakina uwezo wakuzalisha majani mengi ya chai.
Kiwanda cha Mponde kilichofungwa mwaka 2013 baada ya wakulima kugoma kuuza majani yao katika kiwanda hicho ambacho kilikuwa kinaendeshwa na Mwekezaji aliyekuwa ameingia mkataba na Chama cha Wakulima wa Chai (Usambara Tea Growers Association – UTEGA).
Kiwanda cha kusindika majani mabichi ya chai cha Mponde kilianza kujengwa mwaka 1969-1970, chini ya Mamlaka ya Chai Tanzania (T.T.A), Mnamo mwaka 1988 kiwanda hicho kilibinafsishwa na kupewa Chama cha Wakulima wa Chai cha Usambara (UTEGA) ambao wamlimtafuta mwekezaji kwa ajili ya kukiendesha.