*************************************************
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Aboubakar Kunenge leo amepokea mchango wa Madawati 400 kutoka Bank ya NMB kwaajili ya kusaidia tatizo la uhaba wa Madawati Jijini humo ambapo ametoa wito kwa Wadau kuendelea kuchangia sekta ya elimu.
RC Kunenge amesema mpaka kufikia siku ya leo Wamefanikiwa kukamilisha Ujenzi wa Vyumba vya Madarasa 97 kati ya 339 kwaajili ya wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato Cha Kwanza na kukosa nafasi ambapo amebainisha Hadi kufikia February 28 madarasa yote yatakuwa yamekamilika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la waziri Mkuu.
Aidha RC Kunenge ameishukuru Bank ya NMB kwa kutoa mchango huo ambao kwa kiasi kikubwa utaenda kupunguza tatizo la uhaba wa Madawati ambapo amesema mbali na ujenzi wa madarasa pia wanaendelea na ujenzi wa Madawati takribani 40,000 ambayo yapo Katika hatua nzuri ya kukamilika.
Akikabidhi Madawati hayo, Kaimu Afisa Mkuu wa fedha wa Bank ya NMB Bwana Benedicto Baragomwa amesema Madawati hayo yatagawanywa Katika Shule mbalimbali ambapo Shule ya Msingi King’ongo itapatiwa Madawati 150 na Madawati yaliyosalia yatakabidhiwa kwa shule nyingine.
Hata hivyo Bwana Baragomwa amesema Bank hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mkoa huo Katika masuala mbalimbali ya kijamii.