Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Madaba mkoani Ruvuma Theofanes Mlelwa aliyevaa kapelo akiangalia moja kati ya nyumba sita za wakuu wa Idara wa Halmashauri hiyo zinazojengwa na Serikali kwa ajili ya kuishi wakuu wa idara ambapo mara zitakapokamilika zitasaidia sana kupunguza changamoto ya wakuu wa idara kuishi mbali na eneo la kazi.
Picha na Muhidin Amri
………………………………………………………………….
Na Muhidin Amri,Madaba
SERIKALI imeipatia Halmashauri ya wilaya Madaba mkoani Ruvuma, kiasi cha shilingi milioni 600 kati ya hizo milioni 300 zitatumika kwa ajili ya kujenga nyumba ya kuishi Mkurugenzi Mtendaji na nyumba sita za wakuu wa idara wa Halmashauri.
Afisa Mipango wa Halmashauri ya Madaba Mwandishi Nchimbi amesema, nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji ni ghorofa 1 na zile za watumishi ambazo gharama yake ni milioni 300 ni za kawaida na ziko katika hatua ya lenta.
Nchi mbi alisema, nyumba hiyo itakapokamilika itamwezesha Mkurugenzi kuwa na makazi bora karibu na ofisi, hivyo kutekeleza majukumu yake ipasavyo pamoja na kuondoka kuishi katika nyumba ndogo iliyojengwa kwa ajili ya mtumishi wa idara ya Afya.
Alisema, ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi na nyumba za wakuu wa Idara zinajengwa kwa kutumia mfumo wa force akaunti ambapo Halmashauri inanunua vifaa na kuwapa mafundi, badala ya utaratibu wa zamani kuwatumia wakandarasi ambao ulichangia kuchelewesha ujenzi wa miradi mingi.
Kuhusu nyumba za wakuu wa idara alisema, zitaongeza morali ya watumishi kufanya kazi kwa kujituma kwani zitamaliza changamoto ya umbali kutoka katika makazi yao hadi ofisi za Halmashauri, jambo lililo sababisha hata baadhi ya watumishi kuhama na kwenda kufanya kazi katika Halmashauri na meneo mengine nchini.
Hata hivyo alisema, changamoto kubwa katika Utekelezaji wa miradi hiyo inajenga kipindi cha masika kwa hiyo wanashindwa kusafirisha vifaa hadi eneo la ujenzi kutokana na magari kukwama na madereva wanalazimika kupaki mbali na mradi na jamii inayowazunguka kutokuwa tayari kwenda kufanya kazi.
Kwa upande wake Mhandisi anayesimamia ujenzi huo Shaban Kasanzu alisema, kwa nyumba ya Mkurugenzi ujenzi umefikia hatua ya kumwaga jamvi na kuhaidi kwamba jengo hilo litakuwa na ubora wa hali ya juu na litakamilika kwa wakati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba Shafi Mpenda alisema, ujenzi umeshaanza na unaendelea vyema ambapo ameishukuru Serikali kuipatia Halmashauri hiyo kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya nyumba 6 za watumishi na nyumba 1 ya kuishi Mkurugenzi.
Alisema, kupitia vikao mbalimbali na wakuu wa idara walikubaliana nyumba hizo kujengwa karibu na ofisi ili kuwarahisishia wakuu wa idara watakaoishi katika nyumba hizo kuwahi kazi na kutekeleza majukumu yao ya utumishi kwa muda muafaka.
Alisema, katika suala la usimamizi na ufuatiliaji wa ujenzi kila nyumba imekabidhiwa kwa mkuu wa idara na msaidizi wake kwa barua ili kusimamia kwa karibu ujenzi na kufahamu changamoto zinazowakabili mafundi.
Alisema, jukumu kubwa la Mkuu wa idara ni kusikia changamoto zilizopo, kutoa maoni yake na kufikisha kwa kamati ya husika ya manunuzi,ujenzi na ufuatiliaji ambazo wajumbe wake ni Mkuu wa wilaya,Mkurugenzi na Afisa Mipango kwa ajili ya kuzipatia majibu ili kuhahakisha nyumba hizo zinakamilika kwa wakati uliopangwa.
Alisema, nyumba hizo zitaleta tija kubwa kwa wakuu wa idara, na kwa mujibu wa kanuni za Utumishi wa Umma, Serikali inatakiwa kuwapa nyumba za kuishi zenye staa wakuu wa idara na kama serikali itashindwa kumpa nyumba basi inawajibu wa kumlipia kodi katika nyumba atakayoishi.
Pia Mpenda alisema, ujenzi wa nyumba hizo utasaidia sana kuokoa fedha ambazo zingetumika kulipia kodi nyumba na watumishi kukaa katika eneo moja ambalo litawaletea heshima kubwa kwa jamii kuliko kuchanganyika na watu wengine.