************************************************
21/01/2021 ZANZIBAR
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro ameitaka jamii husasani inayoishi katika visiwa vya Unguja na Pemba, kuacha kujihusisha na vitendo vya udhalilishaji kwani Jeshi la Polisi kamwe halitosita kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuwafikisha mahakamani.
IGP Sirro amesema hayo leo wakati alipofanya ziara ya ukaguzi Kisiwani Zanzibar ziara ambayo imelenga kufanya tathimini, changamoto na mafanikio wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika visiwani humo.
Aidha, IGP Sirro ameendelea kukemea baadhi ya vitendo vinavyofanywa na wahalifu wachache wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kwamba Jeshi la Polisi bado litaendelea kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
Wakati huo huo IGP Sirro amekutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati alipomtembelea ofisini kwake Ikulu Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha rasmi kwa Mhe. Rais ambapo Dkt. Mwinyi amelipongeza Jeshi hilo kwa utendaji kazi mzuri.