Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa nasaha kwa wadau wa mazingira alioambatana nao wakiwemo viongozi wa dini katika siku ya Upandaji miti kimkoa inayofanyika kila tarehe 19 mwezi Januari
Miongoni mwa Wadau wa Mazingira akiwemo afisa Zana za kilimo ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa Sebastian Kioyo pamoja na Kaimu Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Ntera wakipanda miparachichi katika Shamba la Gereza la Mollo Manispaa ya Sumbawanga.
Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Justin Malisawa (kulia) akiwa na wadau wengine katika siku ya upandaji miti na uzinduzi wa upandaji miti ya matunda katika mkoa wa Rukwa wakiwa katika shamba maalum la kupanda miparachichi katika Gereza Mollo.Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (aliyeshika Jembe) akimalizia kufukia mparachichi alioupanda kati ya miparachichi 100 iliyopandwa katika shamba la Gereza Mollo Manispaa ya Sumbawanga akiwa pamoja na wadau wengine walioshiriki katika uzinduzi wa upandaji wa miparachichi.
***********************************************
Mkuu wa mkoa wa rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa siku tatu kwa wakurugenzi wa Halmshauri za Mkoa wa huo kujieleza kwa maandishi sababu za kushindwa kutekeleza maagizo ya Makamu wa Rais wa Tanzania Mheshmiwa Samia Suluhu Hassan yaliyotolewa mwaka 2015 ya kuzitaka halmashauri nchini kupanda miti isiyopungua milioni 1.5 kila mwaka ili kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Akifafanua kutoridhishwa huko Mh. Wangabo amesema kuwa kwa kipindi cha mwaka 2018/2019 halmashauri nne za Mkoa wa Rukwa zilipanda miti milioni 2.5 ambayo ni sawa na 43% huku mwaka 2019/2020 halmashauri hizo zikipanda miti milioni 1.6 ambayo ni sawa na 26% wakionesha kushuka maradufu katika utekelezaji wa agizo hilo na kuongeza kuwa hali hiyo haikubaliki na hivyo kuwaagiza wakurugenzi hao kutoa taarifa ya maandishi kueleza sababu za kushindwa kutekeleza agizo hilo.
“Tangu Mwaka 2015 ‘trend’ ya upandaji miti inashuka chini sasa tupo kwenye asilimia 26 ya miti milioni 6, tumepanda milioni 1.6 kwa mkoa mzima, lakini uharibifu wa mazingira huko ni kubwa sana, uharibifu wa ukataji wa miti ni mkubwa, kwa shughuli za mifugo, shughuli za ujenzi, shughuli za mkaa, miti inaangamia lakini hatupandi inayolingana na tunayoikata,” Alisema
Aidha aliongeza kuwa taarifa hiyo iambatane na mpango kazi wao unaoonesha kujipanga kwa utekelezaji wa agizo hilo kuanzia mwezi januari mwaka huu, mpango ambao utaonesha upandaji na usimamizi wa miti hiyo mpaka mwezi wa nne mwaka 2021 na kisha kuwataka wakuu wa wilaya kufanya ukaguzi katika halmashauri zao ili kuhakikisha kwamba kila halmashauri imepanda miti milioni 1.5 na inasimamiwa.
“Mimi mwenyewe nimeonesha njia hapa leo tu tumepanda miti Zaidi ya 100, sasa kinashindikana kitu gani huko, wenyeviti wa vitongoji wapo huko, wenye viti wa vijiji wapo, watendaji wa vijiji na kata wapo, Tarafa wapo, maafisa ugani wote wapo, taasisi za shule zipo chungumzima, hizi tu peke yake ukizisimamia zikapanda miti mbona miti ni imgi sana, lakini juu ya yote kuna wadau wa mbalimbali wa mazingira tunao hapa,” Alisisitiza.
Mh. Wangabo ameyasema hayo katika siku ya upandaji miti kimkoa inayofanyika tarehe 19 ya Mwezi wa kwanza kila mwaka huku akizindua rasmi upandaji miti ya matunda hasa miparachichi katika Gereza la Mollo na Kijiji cha Malonje kwaajili ya kuimarisha vipato vya gereza na wananchi kuwa na zao mbadala la kilimo kwaajili ya biashara, tukio ambalo limekusanya wadau mbalimbali wa mazingira Pamoja na viongozi wa dini mkoani humo.
Akitoa taarifa fupi ya upandaji wa miti katika Gereza la Mollo Manispaa ya Sumbawanga Mkuu wa Gereza hilo SP Englibert Chingalo alisema kuwa gereza lilipokea miche 655 kutoka ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Rukwa hadi kufikia tarehe 14.1.2021 na kusema “Tangu gereza la Mollo lianzishwe mnamo mwaka 1967 haijawahi kupandwa bustani ya miche ya matunda kama inavyofanyika leo, aidha miti hii ya matunda itakuwa ni faida kubwa kwa wafungwa, watumishi wa gereza Mollo Pamoja na jamii nzima inayotuzunguka.”
Kwa upande wake Meneja wa Msitu wa Mbizi Mkoani Rukwa Mohamed Kiangi alimuomba Mkuu wa Mkoa huo kuboresha program hiyo aliyoianzisha kwa kuhakikisha inakuwa na usimamizi bora wa miti inayopandwa hasa katika taasisi za serikali Pamoja na kwa wananchi kwa kuwa na takwimu za wapandao miparachichi hiyo huku halmashauri zikichangia gharama za uzalishaji wa miche kwa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) mkoani humo ili wakala hao wawe kitalu cha kuzalishia miti hiyo.
Aidha kwa upande wao viongozi wa dini, wamesifu juhudi zinazofanywa na Mkuu wa Mkoa huo katika kuhamasisha upandaji wa miti ya matunda na kulifananisha tendo hilo na ibada na hivyo kumuomba asichoke kuendelea kuwahimiza wananchi kupanda miti hiyo ya matunda.
Askofu wa Kanisa la KKKT Ambele Mwaipopo wa Dayosisi ya Ziwa Tanganyika kwa mkoa wa Rukwa na Katavi alisema, “Mwenyezi mungu alipomuweka mwanadamu katika bustani ya Edeni alimuweka katika mazingira yaliyorafiki kwaajili ya kuendeleza uhai wake kwahiyo tendo hili la upandaji wa miti nit endo la kiibada, tendo la sifa na tuzo kwa Mwenyez Mungu, Kwahiyo tuko Nyuma yako mkuu wa Mkoa tutatangaza kwenye makanisa yet una misikiti yet una maeneo yetu ya ibada.”
Naye Katibu wa Baraza la Kuu la Waislamu (BAKWATA) Mkoani Rukwa alisema, “Kama alivyosema Baba Askofu Mwaipopo kwamba sisi kama viongozi wa dini jambo hili tumelichukua na tutalitangaza katika nyuma zetu za ibada makanisani na misikitini kuwahamasisha waumini wetu kupanda zao hili la miparachihci Pamoja na mazao mengi ne tukushukuru Mkuu wa mkoa kwa kuhamasisha mazao haya ambayo tulikuwa hatuyapi kipaumbele.”
Akizungumza kwa niaba ya wadau wa mazingira mkoani humo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mazingira Mkoani Rukwa Kapteni Mstaafu Mzee Zeno Nkoswe alisema kuwa mazingira ya Mkoa yamerudi nyuma na kuongeza kuwa kuna uwazi Zaidi ya km 200 kuanzia Kijiji cha Tunko Wilayani Sumbawanga hadi mji mdogo wa Namanyere Wilayani Nkasi.
“Tunafikiria kazi hii uliyoianzisha itatupa tena nguvu ya kuelimisha wananchi wetu kuhifadhi na kupanda miti na sisi NGO’s zetu Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tunakuunga mkono kwa asilimia zote katika suala hili na tuziombe taasisi hasa za dini tusaidieni makanisani kuwaelimisha wananchi juu ya upandaji wa miti na uhifadhi wake,” Alisema.
Mti mmoja wa parachchi unakadiriwa kuzalisha matunda 500 huku bei ya tunda moja inakadiriwa kuwa Shilingi 500 na hivyo miparachichi 100 iliyopandwa katika Shule ya Msingi Malonje inakadiriwa kuzalisha matunda 50,000 ambayo thamani yake ni shilingi milioni 25 ambazo zinategewa kupatikana baada ya miaka mitatu, fedha ambayo inategemea kutumika katika matumizi mbalimbali ya shule hiyo.