Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari Mjini Babati.
*************************************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU imewafikisha Mahakamani waliokuwa viongozi sita akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilombero Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwa shataka la kuuza ekari 810 bila idhini ya mkutano Mkuu wa Kijiji.
Hata hivyo, washtakiwa wawili hawakuwepo Mahakamani hapo hivyo wanaendelea kutafutwa ili waunganishwe na wenzao kwenye kesi hiyo.
Washtakiwa hao wanne wamefikishwa kwenye mahakama ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Charles Uiso na kusomewa mashtaka hayo na mawakili wa TAKUKURU, Adam Kilongozi na Martin Makani, leo January 20.
Washtakiwa wa kesi hiyo namba 12/2021 ni ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Emmanuel Komba, aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji hicho Jamhuri Munna na waliokuwa wjumbe wanne wa serikali ya kijiji hicho.
Wajumbe hao ni Habibu Dimbui, Robert Matua, Sara Isack na Hatibu Rajabu.
Waendesha mashtaka hao, wamedai kwamba mshtakiwa Komba aliuza ekari 400 yaa ARDHI bila idhini ya mkutano Mkuu wa kijiji na kuwezeshwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho Munna kujipatia faida isiyomstahili ya shilingi milioni 114.5.
Wajumbe hao wanne wanatuhumiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kuidhinisha mauzo ya ekari 400 kinyume cha kifungu cha 31 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007.
Hata hivyo, washtakiwa hao wamekana mashataka hayo mahakamani hapo na wamepelekwa mahabusu mara baada ya kushindwa kupata dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi itakapotajwa tena Januari 21 mwaka huu mahakamani hapo.
Washtakiwa wawili Komba na Dimbui ambao hawakuwepo mahakamani hapo wanaendelea kutafutwa ili kuunganishwa kwenye kesi hiyo.
Mkuu wa TAKUKURU mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu amedai kuwa uchunguzi wa TAKUKURU umeonyesha Wilaya za Simanjiro na Kiteto na Kiteto, kumezuka mtindo wa viongozi wa vijiji wakiwemo wenyeviti, watendaji na wajumbe wa kamati ya ardhi kujipa mamlaka ya kuuza au kusimamia uuzaji ardhi ya kijiji bila idhini ya mkutano mkuu wa kijiji.
Ametoa rai kuwa katika uuzaji wa ardhi, wenyeviti wa vijiji, wajumbe wa kamati za ardhi wazingatie sheria ya ardhi ya vijiji CPA 114 ambapo kijiji kupitia mkutano mkuu wa kijiji umepewa mamlaka ya kuuza ekari 50 na siyo vinginevyo.
Makungu amesema wanaonunua ardhi hiyo kupitia uongozi wa kijiji bila kupitia mkutano mkuu wa kijiji wafahamu kuwa wanalaghaiwa na mikataba ya uuzaji huo ni batili.
“Kila tunapowabaini wafahamu kuwa watapoteza fedha zao kutokana na manunuzi hayo batili mbele ya sheria ya ardhi hivyo itarejeshwa kwenye umiliki wa vijijin husika,” amesema Makungu.