Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara Holle Joseph Makungu akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Naisinyai Wilayani Simanjiro kwenye mkutano wa kuwajengea uwezo juu ya rushwa na kusikiliza kero mbalimbali kupitia ofisi ya TAKUKURU inayotembea.
************************************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, imeanzisha mpango wa kusikiliza kero za wananchi kwa kuwafuata vijijini kupitia ofisi inayotembea (mobile office) ili waweze kuwafikia kwa wingi zaidi.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Makungu aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Naisinyai wilayani Simanjiro.
Makungu amesema kwa kuanzia wamefikia kijiji cha Naisinyai na kusikiliza kero na changamoto mbalimbali za wananchi Kisha wataendelea na vijiji vingine vya mkoa wa Manyara.
“TAKUKURU tumeona hakuna haya ya kukaa ofisini ila kupitia mobile ofisi tutaweza kuwafikia wananchi wengi zaidi na kusuluhisha changamoto zilizopo na kufuatilia nyingine kwa ukaribu zaidi,” amesema Makungu.
Amewataka wakazi wa eneo hilo kutoa kero, changamoto na matatizo yao bila hofu yoyote kwani hakuna mtu au kiongozi ambaye atawahoji baada ya kuwasilisha hoja zao.
Mwenyekiti wa kijiji cha Naisinyai, Merika Makeseni amesema wananchi wa eneo hilo wanaamini katika mazungumzo na siyo kulalamika pindi wakiwa na kero zao.
“Tuna matumaini kuwa kero mbalimbali zilizofikishwa na wananchi kupitia TAKUKURU zitafanyiwa kazi na kupatikana ufumbuzi wake,” amesema Makeseni.
Amesema wanawakaribisha tena TAKUKURU baada ya miezi sita au mwaka mmoja warudi na majibu ya ufumbuzi wa kero mbalimbali za wananchi zilizotolewa kwenye mkutano huo wa TAKUKURU inayotembea.
Mkazi wa kijiji cha Naisinyai John Mollel amesema wamehitimu mafunzo ya mgambo tangu mwaka 2017 ila hawajapatiwa vitambukisho na vyetu vya kuhitimu.
Mkazi mwingine Isack amesema baadhi ya askari wanaolinda ukuta unaozunguka machimbo ya madini ya Tanzanite wanawapiga raia na kunyan’ganyana wanawake wao.
Mkazi mwingine Aloyce Kiroia amesema kuna kigogo mmoja anafanya utaratibu wa kuchukua ardhi ya kijiji hicho hivyo achukuliwe hatua kali.