Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akifungua Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma leo Januari 19,2021.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizindua Vitabu vya Mkakati na Muongozo wa kufundishia Lugha ya Kiswahili kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili yaliyoadhimishwa leo Januari 19,2021 katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi, Wajumbe, Wadhamini na Wafanyakazi wa Taasisi za Kiswahili baada ya Kufungua Maadhimisho ya Siku ya kiswahili katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma Leo Januari 19,2021.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiagana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Seikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Tabia Maulid Mwita na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Abdalla Ulega baada ya Kufungua Maadhimisho ya Siku ya kiswahili katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma Leo Januari 19,2021.
(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa Maagizo kwa Wizara ya Wizara ya Habari ,utamaduni Sanaa na Michezo Ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wizara ya Habari Zanzibar kuhakikisha zinakaaa na wataalam ili Kiswahili kitumike katika nyaraka mbalimbali za Serikali ikiwemo hukumu za mahakama.
Mhe.Suluhu ametoa maagizo hayo leo Januari 19,2021 jijini Dodoma katika maadhimisho ya Kiswahili yaliyoanza leo Januari 19 ,2021 na kutarajia kuhitimishwa kesho Januari 20,2021 ambapo pia ameagiza kushirikiana na mabaraza ya Kiswahili[BAKITA na BAKIZA]na kuja na mikakati ya pamoja katika kukuza Kiswahili kwa kuandaa wataalam wa Kiswahili.
Aidha,Makamu huyo wa Rais amesema Taasisi za kuendeleza lugha ya Kiswahili [BAKITA na BAKIZA] ni muhimu kukumbukwa kwa kupatiwa fedha huku akitoa msisitizo kwa sekta binafsi kuchapisha machapisho ya Kiswahili.
Pia,Mhe.Suluhu amebainisha kuwa Mapinduzi ya viwanda yatumike katika mfumo wa Kiswahili hususan kwenye mfumo wa kidijitali[TEHAMA].
Hata hivyo Mhe.Suluhu amesema Kiswahili kinaiunganisha Tanzania na mataifa mbalimbali katika kukuza uchumi wa nchi na uhusiano mzuri wa kimataifa ambapo ni jambo la kujivunia huku tafiti mbalimbali zimekuwa zikifanyika na kubainisha kuwa zaidi ya watu milioni 100 hadi 150 duniani wanatumia lugha ya Kiswahili vyombo vya Habari vikitajwa kuwa na mchango mkubwa katika kueneza Kiswahili.
Makamu huyo wa Rais ameendelea kufafanua kuwa Licha ya mafanikio ya Kiswahili bado kuna changamoto mbalimbali zikiwemo uhaba wa vitabu vya kufundishia wageni,upungufu wa wataalam wa kufundisha Kiswahili kwa wageni.
Kwa upande wake Naibu Waziri Wizara ya Habari ,Utamaduni ,Sanaa na Michezo Abdallah Ulega amesema Wizara imeandaa Kanzi data ya wataalam wa Kiswahili ambapo hadi sasa kuna jumla ya Wataalam 1308 wapo katika kukiendeleza na kukikuza Kiswahili.
Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili la Taifa [BAKITA ]Dkt.Mathew Samwel amesema tuzo zitakazotelewa katika maadhimisho haya ni pamoja na tuzo kwa mwandishi wa vitabu vingi vya Kiswahili,Mwanafunzi bora ,vyombo vya Habari vinavyofanya vizuri katika lugha ya Kiswahili na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kutunukiwa nishani ya juu ya Shaban Robert kwa kuendeleza Kiswahili.
Chimbuko la Maadhimisho ya Kiswahili Tanzania ni tarehe 31,Julai,1992 kijiji cha Kwembe Jijini Dar Es Salaam ili kuendeleza lugha adhimu ya Kiswahili ambapo kwa mwaka huu yanakwenda sambamba na kaulimbiu isemayo bidhaisha Kiswahili kwa maendeleo Endelevu ya Tanzania.