Mkuu wa shule ya sekondari Mirerani B.W.Mkapa ya Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Samwel Kaitira akisoma matokeo ya kidato cha pili na cha nne yaliyofanyika mwaka jana ambapo shule hiyo imefaulisha kwa kiwango kizuri.
***********************************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WADAU wa maendeleo wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamewapongeza walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Mirerani B.W. Mkapa kwa ufaulu mzuri wa matokeo ya kidato cha pili na cha nne.
Wadau hao wameipongeza shule hiyo baada ya kuongoza kwenye wilaya nzima ya Simanjiro kwa kuwa shule ya kwanza katika kufaulisha kupitia matokeo ya kidato cha pili na cha nne yaliyofanyika mwaka jana yaliyotangazwa hivi karibuni.
Makamu Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani, Christopher Chengula amesema wapo mbioni kufanya jambo kwa walimu wa shule hiyo ili kuwapa hamsa ya kufundisha zaidi wanafunzi wa shule hiyo.
“Sisi kama viongozi wa mamlaka ya Mji mdogo tunawapongeza walimu, wazazi na wanafunzi wa shule hiyo kwa ufaulu mzuri kwani wameipa sifa shule hiyo na kuitangaza vizuri,” amesema Chengula.
Diwani wa kata ya Endiamtu, Lucas Zacharia amesema walimu wa shule hiyo wamefanya kazi kubwa hadi kufaulisha kwa kiwango hicho wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne.
“Hii ni changamoto kwetu ili kuhakikisha wazazi na walezi wanatumia nafasi yao kutimiza mahitaji na ninyi walimu kubaki na kazi ya taaluma tuu,” amesema.
Mkuu wa shule ya sekondari Mirerani B.W. Mkapa, Samwel Kaitira amesema kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne na cha pili kinazidi kupanda baada ya matokeo hayo kutangazwa hivi karibuni.
Kaitira amesema kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa hivi karibuni ya kidato cha nne, wanafunzi tisa walipata daraja la kwanza, 27 walipata daraja la pili, 21 daraja la tatu, 63 daraja la nne na daraja sifuri ni 32.
“Kwa upande wa kidato cha pili wanafunzi 38 walipata daraja la kwanza, 29 daraja la pili, 47 la tatu, 58 la nne na wanafunzi wawili walipata daraja sifuri,” amesema Kaitira.
Ofisa mtendaji wa Kata ya Endiamtu, Charles Msangya amewapongeza walimu wa shule hiyo kwa ufaulu mzuri wa matokeo ya kidato cha nne na cha pili yaliyotangazwa hivi karibuni ila wasirudi nyuma waendelee kuwa imara zaidi.
“Tunawapongeza walimu wetu wa Mirerani B.W. Mkapa kwa hatua hii kwani mnasababisha morali kwa wengine kufanya vizuri zaidi kwenye mitihani yao inayokuja kufanya vizuri zaidi,” amesema Msangya.
Ofisa Tarafa wa Moipo Joseph Mtataiko amewapongeza walimu wa shule hiyo na wanafunzi kutokana na matokeo mazuri ya ufaulu wa mitihani ya kidato cha nne na cha pili.
“Ufaulu huu ni matokeo ya kambi mliyoweka kwa kuhakikisha wanafunzi wanasoma hadi usiku, wale wazazi waliokuwa wanapinga hilo watoto wao ndiyo wamefeli sasa,” amesema Mtataiko.
MWISHO