Mwenyekiti wa mtandao wa wakulima mkoa wa Arusha Mchungaji John Safari akisoma Tamko la kuipongeza serikali mbele ya waandishi wa habari hawapo pichani mapema jana jijini Arusha picha zote na Ahmed Mahmoud Arusha
Mratibu wa mtandao wa Wakulima mviwata mkoa wa Arusha Richard Masandika akionyesha Mbegu za Asili ambazo Bado hazijafanyiwa GMOS wakati wakitoa Tamko la kuipongeza Serikali jijini Arusha
Sehemu ya mbegu za Asili ambazo bado hazijafanyiwa utafiti wa Majaribio ya Uhandisi-jeni (genetically modified organisms- GMOs) serikali inataka zifanyiwe utafiti hapa nchini picha zote na Ahmed Mahmoud Arusha .
********************************************
Na Ahmed Mahmoud Arusha
Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji vya Mikoa ya Arusha,Manyara Kagera Morogoro,Kilimanjaro Ruvuma na Kagera Women Environmental Society, kwa pamoja wamepongeza na kuiunga mkono serikali kwa msimamo uliotolewa January 13 wa kufuta majaribio ya uhandisi jeni.
Msimamo huo wa serikali uliotolewa tarehe 13 Januari 2021 na Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda, akiwa katika ziara ya kikazi kutembelea kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) kilichopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam ndio imewaibuwa wadau hao na kuipongeza serikali kwa hatua hiyo
Kauli hiyo imelenga agizo la Serikali kufutwa kwa Majaribio ya Uhandisi-jeni (genetically modified organisms- GMOs) yaliyokuwa yakifanyika nchini na msisitizo uliotolewa na Serikali kwamba Taasisi za Utafiti wa Kilimo kwa Sasa zijikite katika kufanya tafiti za kuboresha mbegu kwa ajili ya kilimo.
Kwa mujibu wa Agizo hill ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa udhibiti wa mbegu za mazao na kuhakikisha mbegu ambazo hazikuhakikiwa ipasavyo hazitumiki kama uchochoro wa kupitisha mbegu zilizofanyiwa uhandisi-jeni hapa nchini.
Akizungumza na vyombo vya habari Mwenyekiti wa mtandao wa wakulima mkoa wa Arusha Mchungaji John Safari amesema kwamba Ni dhahiri kuwa kauli ya serikali, siyo tu imekusudia kutoa hakikisho la uhuru wa mbegu na uhuru wa chakula (seed sovereignty and foodovereignty) kwa taifa lakini pia imelenga kulinda uhuru wa kujiamulia mambo kama taifa.
“Sisi wakulima wadogo tunaichukulia kauli hiyo iliyotolewa na Waziri wa Kilimo kama tangazo la wazi la “kulinda uhuru wetu” dhidi ya wale wote wanaofanya ushawishi wa wazi na wa kificho kwa watendaji serikalini na kwa wanasiasa ili kuruhusu majaribio ama uingizaji wa mbegu zilizofanyiwa uhandisi-jeni (GMOs).
“Kwa muda mrefu, sisi wakulima wadogo ambao ndio wazalishaji na walishaji wa taifa letu, tumeshuhudia kuwepo kwa jitihada mbalimbali toka kwa baadhi ya mawakala wa mashirika makubwa ya nje yanayomiliki teknolojia na kufadhili tafiti za GMO katika mataifa mbalimbali ulimwenguni”alisema John Safari ”
Amesema kwa muda mrefu wameshangazwa na “wema huo uliopitiliza” kutoka kwa makampuni hayo yanajulikana kwa kutokuwa na chembe ya rekodi ya wema kwa nchi na jamii maskini ulimwenguni zaidi ya kuwa wameandaa fursa na watengeneza faida wasiojali utu na ubinadamu.
Aidha amefafanua kuwa Wakulima wadogo wamefarijika sana na kauli ya Waziri, ambaye mbali na kutoa msimamo wa serikali kuhusiana na mbegu zilizofanyiwa uhandisi-jeni (GMO), alielezea pia umuhimu na nafasi ya mbegu za asili katika kutoa hakikisho la upatikanaji wa mbegu ambazo zimekuwa chanzo na tegemeo kwa uhuru na uhakika wa chakula nchini.
Alibainisha kuwa Wakulima wadogo wamechukulia kauli ya serikali kupitia Waziri wa Kilimo, kama itikio la serikali kufuatia kilio cha muda mrefu cha wakulima wadogo kuzitaka mamlaka husika kuzitambua na kusaidia kuziendeleza mbegu za asili zilizorithiwa toka vizazi hadi vizazi na ambazo zimekuwa chanzo kikuu cha uhakika na usalama wa chakula kwa taifa
Safari alisema wao Kama Wakulima wadogo wanatambua nafasi ya vyama vya wakulima wadogo na nafasi ya uhuru wa mbegu kwa uendelevu wa taifa na kuipongeza serikali kwa hatua iliyochukua
Mwenyekiti amesema Mara baada ya kauli hiyo wamependekeza Kufanyika kwa mapitio ya sera na sheria zinazohusiana na mbegu ili kuhakikisha kuwa mbegu za asili zinatambulika, zinalindwa na Kuziba mianya yote ya kisera na kisheria inayotoa fursa ya kufanyika kwa majaribio ya mbegu za GMO hapa nchini,
Kwa upande wake mratibu wa mtandao wa Wakulima mviwata mkoa wa Arusha Richard Masandika alisema kwamba umuhimu wa mbegu za asili kwa Wakulima ni kufikia kilimo Cha asili chenye tija bila kutumika mbegu za kisasa na kuwepo na uhakika wa chakula
Alisema kwa muda mrefu Wakulima wamelilia kutumika mbegu za asili lakini hawakuweza kufanikiwa Ila kwa Sasa Wakulima watarajie neema kubwa katika kutumika mbegu za asili katika kilimo baada ya kauli ya waziri kilimo
Makamu mwenyekiti Anna Ephata ameshukuru kwa tamko la Waziri na kusisitiza kuendelea Kufanyika utafiti na kuelimishwa kwa Wakulima kutumia mbegu za asili kwani Zina stahimili magonjwa na kuzaa mazao mengi
Alisema mbegu za asili mkulima akitumia kitaalam zina muondolea gharama ambazo sio za lazima kwenda kununua mbegu Mara kwa Mara na wengi wao hufunga Safari kwenda mjini kupata mbegu hizo kama ilivyokuwa awali miaka ya nyuma.