Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga (kati kati), akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi Ngusa Julius (kusoto), wakati alipotembelea eneo la Jangwani, jijini Dar es salaam, kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu katika neo hilo.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi Ngusa Julius, akimuonesha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga (watatu kulia), kazi zinazofanyika kwa sasa wakati wakati alipotembelea eneo la Jangwani, jijini Dar es salaam, kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu katika eneo hilo.
Zoezi la utoaji mchanga likiendelea katika eneo la Jangwani, jijini Dar es salaam, ambalo linatekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) jijini humo, ili kusaidia kupunguza athari za mafuriko katika eneo hilo.
Muonekano wa daraja la Jangwani, jijini Dar es salaam, ambapo kwa sasa zoezi la utoaji mchanga linafanyika katika daraja hilo ili kuzuia athari za mafuriko ambazo zinapelekea uharibifu wa miundombinu hiyo.
PICHA NA WUU
……………………………………………………………………………….
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi Ngusa Julius, kuhakikisha anendelea na shughuli za utoaji mchanga katika mto Msimbazi eneo la Jangwani, jijini Dare es salaam, ili kudhibiti changamoto zinazoweza kujitokeza hususani kipindi cha mvua.
Akizungumza mara baada ya kukagua na kuridhishwa na kazi inayoendelea katika eneo hilo, Mwakalinga amemwagiza Meneja huyo kuandaa mchoro ambao utasaidia ufanisi wa kazi hiyo ili kutambua na kuyatafutia ufumbuzi maeneo yote yenye changamoto kubwa hasa kipindi cha mvua.
“Sisi kazi yetu si kupambana na maji, kazi yetu ni kuchimba eneo hili na kuelekeza maji sehemu ya kwenda, tunafanya hivi ili kupunguza athari za maji katika eneo hili”, amesema Mwakalinga.
Mwakalinga, pia amemuagiza Mhandisi Ngusa kufanya matengenezo mara kwa mara ili kuepusha Serikali kutumia gharama kubwa ya kufanya matengenezo ya miundombinu mara baada ya matatizo kutokea.
Kuhusu suala la mpango wa ujenzi wa daraja kubwa katika eneo hilo, Mwakalinga, amesema kuwa mpango huo unaendelea vizuri na mchoro huo ukikamilika basi kazi hiyo itaanza mara moja.
Aidha, Mwakalinga amesisitiza kuwa kwa sasa mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa inakagua miundombinu yake yote ili kuhakikisha kunakuwa na usalama wakati wote.
Katika hatua nyingine, Mwakalinga, amekagua daraja la Pugu Kinyamwezi, Manispaa ya Ilala, ambapo amemtaka Meneja wa TANROADS mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na uongozi wa Manispaa hiyo kuhakikisha wanapata ufumbuzi kuhusu kalvati la daraja la Pugu Kinyamwezi ambalo linatiririsha maji kwenye makazi ya watu.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi Ngusa Julius, ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo ya Katibu Mkuu huyo na kusisitiza kuwa bado wanaendelea kusubiri ufumbuzi wa kudumu katika eneo hilo mara baada ya mchoro kukamilika.
“Hapa tunachokifanya kwa sasa ni kufanya matengenezo ya dharura ili kupunguza athari kwa wananchi na watumiaji wa barabara hii, wakati huo huo tukisubiri mwarobaini katika eneo hili”, amesema Julius.
Arch. Mwakalinga, amemaliza ziara yake ya siku moja mkoani Dar es salaam ambapo pamoja na mambo mengine amekagua barabara ya Pugu- Manerumango (Km 60.14) ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami.