…………………………………………………………………………………………
NI Kazi Tu! Hii ni kauli ya Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi kila kata anayofika katika ziara yake ya kutatua changamoto za wananchi wake kwenye kata 16 za jimbo hilo ambapo ametoa Sh Milioni 10 kwenye kata tatu alizozitembelea.
Mbunge Kunambi ambaye alianzia ziara yake kwenye kata ya Uchindile amefanya ziara katika kata tatu za Namwawala, Mbingu na Igima ambako kote huko ametoa mchango wake kwenye maeneo tofauti ikiwemo Elimu, Afya, Miundombinu na Ofisi za Kijiji.
Akizungumza katika Kata ya Namwawala Mbunge Kunambi ametoa mifuko 22 ya saruji na nondo 15 kusaidia ujenzi wa ofisi ya kijiji, mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari ya Namwawala na mifuko 50 ya saruji kusaidia ujenzi wa Zahanati ambapo michango yote hiyo inagharimu kiasi cha Sh Milioni 3.5.
Akiwa katika kata ya Mbingu wananchi na viongozi wa kata hiyo walimueleza changamoto wanayokutana nayo katika kukamilisha ujenzi wa ofisi ya kijiji pamoja na ujenzi wa Sekondari ya kata hiyo.
” Hapa Mbingu ninajua changamoto yenu ni kwenye ujenzi wa Ofisi ya Kijiji cha Chiwachiwa hivyo ninatoa Sh Milioni Moja kwa ajili ya Ofisi hii ambayo ni msaada kwa wananchi wetu wa hapa lakini ninajua jitihada mnazozichukua kwenye ujenzi wa darasa hapa Sekondari yetu ya Mbingu hivyo mimi kama Mbunge ninatoa Sh Milioni 2.3 ili kusaidia ujenzi huo na pale mtakapokwama Diwani nieleze ili mimi kama Mbunge nitoe nguvu yangu,” Amesema Kunambi.
Katika ziara hiyo pia Mbunge Kunambi ametatua changamoto ya Vyoo katika Sekondari ya ambapo ametoa Sh Milioni 2 na mifuko 40 ya kusaidia ujenzi wa Zahanati ya Mpofu.
” Lengo langu ni kuwa Mbunge ambaye nitaacha alama kwenye Jimbo hili, kuhakikisha kila kata iliyopo ndani ya jimbo langu naigusa kwa usawa ule ule, niwaombe madiwani wangu tufanye kazi kwa kasi na nguvu ili tumsaidie kazi Rais wetu Dk John Magufuli ya kuwatumikia watanzania ambao walituchagua.