Sehemu ya Jengo la Utawala la Halmashauri ya wilaya Madaba mkoani Ruvuma likiwa limekamilika kwa asilimia 99 na limeanza kutumika kwa watumishi wa Halmashauri hiyo kutekeleza majukumu yao ya kila siku.Jengo hilo limegharimu zaidi ya shilingi bilioni 3 linakusudia kuboresha mazingira ya kufanyia kazi watumishi.
Picha na Muhidin Amri
………………………………………………………………..
Na Muhidin Amri,Madaba
MKURUGENZI wa Halmashauri ya wilaya Madaba mkoani Ruvuma Shafi Mpenda amesema, ujenzi wa jengo la utawala kwa ajili ya watumishi wa Halmashauri hiyo hadi sasa limekamilika kwa asilimia 99.
Mpenda amesema hayo jana wakati akizungumza na Habarileo ofisini kwake na kumshukuru Rais Dkt John Magufuli kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni 3 kwa ajili ujenzi wa jengo hilo ambalo kwa sasa limesaidia sana watumishi wa idara mbalimbali kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi mkubwa.
Alisema,walipokea fedha za mradi kwa mafungo ambapo mwaka 2016 walipokea shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga msingi na nguzo za kusimamisha kuta za jengo.
Mpenda alibainisha kuwa,ujenzi rasmi ulianza Mwezi Septemba 2017 baada ya kusaini mkataba na wakala wa majengo Tanzania(TBA) wa shilingi milioni 493 na shilingi milioni 7 zilitumika kwa ajili ya kufanya vipimo vya udongo kwenye eneo la mradi.
Alisema, Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani ilihusika kulipa fidia ya shilingi milioni 6.78 kwa wananchi waliokuwa wamiliki halali wa eneo lililotumika kujenga jengo.
Hata hivyo, Serikali iliendelea kutoa fedha na kufikiwa kiasi cha shilingi bilioni 3 ambazo mpaka sasa Halmashauri imeshazipokea na kutumia shilingi bilioni 2.9 na kubakiwa milioni 85.
Aidha alisema, Mwezi Mei 2020 Halmashauri ililazimika kuvunja mkataba na Tba kutokana na changamoto zilizojitokeza ikiwemo kusua sua kwa ujenzi wa mradi huo ambapo TBA ilijenga Boma tu, hivyo Halmashauri iliomba kibali Tamisemi kwa ajili ya kumalizia ujenzi kwa kutumia mafundi wa ndani(force account)kwa kuamini kwamba utaratibu huo utasaidia kukamilisha mradi.
Kwa mujibu wa Mpenda,baada ya kuomba kibali cha Katibu Mkuu Tamisemi na Halmashauri iliendelea kujenga jengo hilo kwa mfumo wa force Akaunti ambao kimsingi umefanikisha kumaliza jengo hilo haraka na idara zote zimeshahamia.
Alisema,walilazimika kuhamia mapema hasa baada ya kupokea watumishi wengi na jengo walililokuwa wanalitumia ni dogo,na hata usalama wa nyaraka za serikali na usalama wa watumishi ulikuwa mdogo hivyo kushindwa kutekeleza baadhi ya majukumu.
Alisema, ni faraja kubwa kuona sasa watumishi wanachapa kazi ya kuwahudumia wananchi wa jimbo la Madaba na maeneo mengine ya nchi licha ya kutokamilika kwa asilimia 100 ambapo kazi ndogo ndogo zilizobaki zinafanyika wakati wakitumishi wakiwa katika jengo hilo na kazi zilizobaki ni kufunga milango, na marekebisho kwa maeneo ya nje kabla ya fundi kurudia kupaka rangi ya mwisho.
Alisema, fedha zilizobaki wameamua kujenga kibanda cha mlinzi aweze kufanya kazi katika mazingira mazuri,kujenga kantini ili kuwasaidia watumishi kupata huduma ya chakula karibu na kuokoa muda wa kazi wa mwajiri ili watumishi wasipate sababu ya kwenda umbali mrefu na kuchelewa kurudi kuchapa kazi.
Alisema, kukamilika kwa jengo hilo kunakwenda kuchochea morali ya watumishi kufanya kazi kama ilivyo dhamira ya serikali ya awamu ya tano na watumishi kuchochea mahudhurio kazini tofauti na siku za ambapo jengo lililotumika lilikuwa dogo na kuvunja hali ya uwajibikaji kwa watumishi.
Pia alisema, sasa kumekuwa na usiri mkubwa kwa watumishi pale anapotekeleza majukumu yake sambamba na kusaidia mtumishi kuona ufahari kuitanga vyema Halmashauri na Serikali ya awamu ya tano kwani jengo hilo lina huduma zote muhimu.
Mpenda alieleza kuwa, jengo hilo limebadilisha taswira na kuongeza thamani ya eneo hilo na sasa wananchi wanaweza kujenga nyumba kwa ajili ya kupangisha watumishi watakopenda kuishi karibu na ofisi.
Amewataka wananchi kutumia fursa ya kuwepo kwa jengo hilo kujenga nyumba za kisasa,kujenga Hoteli,kumbi za sterehe na miradi mingine ya kuwaingizia kipato kwa sababu Serikali imeshasogeza fursa katika meoneo yao.