*******************************************
Happy Lazaro,Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya amevitaka vyuo mbalimbali vya ufundi nchini kuhakikisha wanawezesha wanafunzi wake kuendeleza bunifu mbalimbali ili ziweze kuwasaidia wananchi na kuleta tija kwao.
Aidha Sabaya alipongeza vyuo vya ufundi nchini kikiwemo chuo Cha ufundi Arusha(ATC) kwa kazi kubwa wanazofanya ya kuhakikisha wanawasaidia wanafunzi kuandaa bunifu zao na kuziboresha ambazo mwisho wa siku zitaleta manufaa kwa jamii katika utatuzi wa changamoto mbalimbali.
Sabaya ameyasema hayo leo katika mkutano wa Kwanza wa jumuiya ya wahitimu wa chuo Cha ufundi Arusha, wenye lengo la kuendeleza ugunduzi walioufanya pamoja na kusaidia wanafunzi waliopo kujifunza juu ya teknolojia za kisasa na baadaye kusaidia jamii inayowazunguka.
“zipo mamlaka ndani ya serikali zinashindwa kuwapa nafasi wanachuo wanaoonyesha bunifu zao ,hali ambayo inasababisha nchi kutokuwa na vijana wazawa wenye uwezo wa kulitumikia Taifa”alisema Sabaya.
Alioongeza kuwa ,ni kazi ya serikali kubeba vijana bunifu wanaoonyesha moyo na utayari katika mambo ya msingi ikiwemo vifaa ambavyo vimebuniwa na vijana wa chuo hicho cha ufundi ambavyo vinawezesha kutatua changamoto mbalimbali.
Sabaya alisema kuwa,ni vyema Nacte na TCU wakakaa pamoja na kuunda bodi moja itakayosaidia vijana wabunifu kufanikisha ugunduzi wao na sio kila mmoja kuwa na vigezo vyake kwani jambo hilo linawarudisha nyuma na kuwakatisha tamaa na kufanya jamii kuendelea kuamini teknolojia za nje.
Mkurugenzi wa elimu ya ufundi kutoka wizara ya elimu, Dokta Noel Mbonde alisema kuwa,ni vyema wanafunzi wanapohitimu chuo wakaendeleza kwa vitendo kile alichokipata kutoka chuoni hapo ili kuonyesha umuhimu wa uwepo wao.
“kitendo cha kuondoka huna chochote ulichokipata chuoni hautakuwa na msaada katika Taifa hili, hivyo natoa rai kujiendeleza na mwishowe kufikia nafasi za juu za uongozi kwani sisi tunapita hivyo mjitahidi nakuacha kujidharau nyie wenyewe kwani serikali hii inajali vijana,”alisema Dkt Noel.
Aliongeza kuwa, ni vyema vijana wasitegemee kuajiriwa bali wajiandae kujiajiri na kwa kufanya hivyo ni lazima wahakikishe wanaigeuza elimu walioipata kuwa ya vitendo zaidi.
Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho cha Ufundi,Issa Suleiman alisema kupitia umoja huo wanafunzi waliomaliza kwenye chuo hicho utasaidia kubadilishana uzoefu na ubunifu mbalimbali walionao lakini changamoto wanayopata ni upatikanaji wa fedha ili kuendeleza taaluma yao.
“Klichopelekea kuzindua jumuiya hii ambayo itasaidia kupata fedha na kuangalia mpangilio wa fedha utakao enda kuendeleza ubunifu unaofanywa na baadhi ya wanafunzi ili kuachana na dhana ya kuuza wazo bali waweze kutengeneza bidhaa zao kamili,”alisema Rais huyo.
Uzinduzi wa jumuiya hiyo ya wanafunzi waliomaliza chuo cha Ufundi Arusha, unatajwa kuwa na manufaa ya kuwafanya wahitimu hao kurudi chuoni na kutatua changamoto zinazoikabili chuo hicho katika nyanja mbalimbali.