Home Michezo IFUENGA UNITED WAJIGAMBA KUIBUKA NA UBINGWA WA ASAS SUPER LEAGUE.

IFUENGA UNITED WAJIGAMBA KUIBUKA NA UBINGWA WA ASAS SUPER LEAGUE.

0

Timu ya Mtwivila ( Ifuenga) United wakiwa katika maandalizi ya moja ya mechi walizocheza ligi ya Asas

**************************************************************

NA DENIS MLOWE, IRINGA

KUELEKEA katika fainali ya kupata bingwa wa soka mkoa wa Iringa inayojulikana kwa jina la Asas Super League kocha wa timu ya soka ya Mtwivila Fc (Ifuenga United), Edger Nzelu amesema kwamba wamejipanga vyema kuchukua ubingwa huo dhidi ya Ivambinungu FC..

Katika fainali hiyo inayotarajiwa kupigwa Januari 17 mwaka huu katika dimba la Samora, Kocha Nzelu alisema kuwa kutokana na kuwa kikosi bora watahakikisha wanachukua ubingwa huo na kuiletea sifa wilaya ya Iringa Vijjini na kuendeleza ubabe wa timu za wilaya hiyo kuchukua ubingwa baada ya msimu uliopita kuchukuliwa na Mafinga Academy.

Alisema kwa kuwa nia ya kuchukua ubingwa ni kutokana na kuwa wachezaji wenye uchu wa mafanikio na lengo la kufika mbali zaidi kisoka hivyo wako katika maandilizi makali kwa ajili ya mchezo huo ambao unatarajia kuwa mgumu kwa kila timu.

Alisema kwamba wako katika maandalizi ya mwisho kuelekea katika mchezo huo na wachezaji wote wako katika hali nzuri kasoro mchezaji mmoja Baraka Duma ambaye ana majeruhi ambayo hayawezi sababisha kuukosa mchezo huo ambao watahakikisha wanaibuka na ubingwa.

Nzelu alisema kuwa wanamshukuru kila mdau aliyejitolea kufanikisha timu hiyo kufika hatua ya fainali hali ambayo watahakikisha wanawapa furaha kubwa kwa kuibuka na ubingwa wa mashindano hayo kwa lengo la kuhakikisha timu inawakilisha mkoa wa Iringa katika mashindano ya mabingwa wa mkoa.

“Tumejipanga vyema kabisa kuhakikisha tunakuwa mabingwa wapya wa msimu huu kwa sababu kwanza tuna kikosi kizuri na tuna wachezaji wazoefu wa kushiriki mashindano haya na bado vijana wadogo wenye nia ya kufanya vyema katika soka nchini” alisema

Aliongeza kuwa hadi kufika hatua ya fainali wamepambana kwa kiasi kikubwa na kwa upande wa  wapinzani watakuwa wamejipanga vyema kwani kila timu inataka kuibuka na ubingwa hivyo kama Ifuenga  wanawaheshimu Ivambinungu FC na wasitarajie mtelemko kutoka kwa vijana.

Aidha alitoa wito kwa mashabiki wa timu ya Ifuenga kujitokeza kwa wingi katika fainali hiyo na kuwataka kuwashangilia kwa nguvu zote kwa lengo la kuwapa nguvu wachezaji na kuwapa hamasa zaidi ya kuibuka na ubingwa katika mchezo huo.

Kwa upande wake nahodha wa kikosi hicho, Tariq Nurdin alisema kuwa wako tayari kwa ajili ya mpambano wa fainali na ahadi waliyowekeana kuibuka na ubingwa lazima itimie kwani wako vizuri kila idara na watahakikisha wanamaliza mchezo ndani ya dk.90.

Ifuenga  ambayo inapewa nafasi kubwa ya kuibuka na ubingwa msimu huu watapambana na Ivambinungu ambao tangu kuanza kwa ligi hiyo wameonyesha ushindani mkubwa hivyo mechi inatarajiwa kuwa nzuri kwa pande zote.

Mashindano hayo ambayo yanatarajia kumalizika Januari 17 yatakuwa na mshindi wa tatu ambapo wapinzani wa jadi timu ya Irole  na Kidamali wataumana vikali kuweza kumpata mshindi wa tatu .

Bingwa ataondoka na milioni 2.5 kikombe cha ubingwa, seti za jezi na mpira na uwakilishi wa kushiriki mabingwa wa mkoa, mshindi wa pili milioni 1.5 mshindi wa tatu laki 7.