WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile,akizungumza wakati akifungua kikao cha utendaji kazi wa Mameneja wa mikoa yote wa Tanzania Bara na Zanzibar wa TTCL na Menejimenti ya Shirika hilo kilichofanyika leo Januari 15,2021 jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi akizungumza kumkaribisha Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile (aliyeketi katikati) kabla ya kufungua kikao cha utendaji kazi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Dodoma. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Waziri Kindamba kilichofanyika leo Januari 15,2021
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) , Waziri Kandamba akitoa taarifa kwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa kikao kazi cha kujadili utendaji wa TTCL kilichofanyika leo Januari 15,2021 jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa kikao wakifatilia hotuba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile (hayupo pichani) wakati akifungua kikao cha utendaji kazi wa Mameneja wa mikoa yote wa Tanzania Bara na Zanzibar wa TTCL na Menejimenti ya Shirika hilo kilichofanyika leo Januari 15,2021 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua kikao cha utendaji kazi wa Mameneja wa mikoa yote wa Tanzania Bara na Zanzibar wa TTCL na Menejimenti ya Shirika hilo kilichofanyika leo Januari 15,2021 jijini Dodoma.
………………………………………………………………………………..
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile amewataka watendaji wa taasisi zilizochini ya Wizara yake kuja na mikakati itakayowezesha taasisi hizo kupiga hatua na kuwa na mafanikio ya haraka na ndani ya siku 100 mikakati hiyo ionekane ya namna ya kuboresha huduma zao.
Dkt.Ndugulile ameyabainisha hayo leo Januari 15,2021 wa kufungua kikao cha utendaji kazi wa Mameneja wa mikoa yote wa Tanzania Bara na Zanzibar wa TTCL na Menejimenti ya Shirika hilo kilichofanyika jijini Dodoma.
Amesema anataka ndani ya siku 100 kuona mambo makubwa yakifanywa ndani ya taasisi za Wizara yake ili kukidhi matarajio ya watanzania katika Wizara hiyo mpya.
“Hakuna kulala hizi siku 100, zikifika tu siku 90 tunataka matokeo yanayopimika na mtendaji wa kila taasisi atakuja mbele yangu kueleza ndani ya kipindi hicho imefanya nini,kinachopimika sio michakato,”amesema Dkt Ndugulile.
Ameongeza kuwa “Inawezekana siku za nyuma hamkuwa na mikataba Kindamba(Mkurugenzi wa TTCL) utakuwa na mkataba na mimi wa performance, utakuja kuniambia nini unakusudia kufanya, nikikubana wewe na wewe utaenda kubanana na wenzako,”amesema.
Aidha ameagiza TTCL kuhakikisha wanapunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuweka mikakati ya kujiendesha kibiashara ili kukidhi soko la ushindani huku bidhaa zao zikipatikana kwa urahisi.
“Kumekuwepo na malalamiko kwa wananchi kama suala la upatikanaji wa vocha baadhi ya mikoa, vocha hazipatikaniki shida ipo wapi?, pia angalieni vifurushi vyenu, nyie mna advantage kuliko kampuni nyingine boresheni vifurushi vyenu,kitengo cha huduma kwa wateja pia kiboreshwe,” amesisitiza.
Hata hivyo Dkt.Ndugulile amewataka kuja na mikakati ambayo ni mizuri tunajua mnamahitaji ya fedha lakini mje na mikakati inayopimika ili hata nikikupa Sh.Milioni 100 basi baada ya muda uniletee Sh.Milioni 300, lengo la Wizara ni kuona TTCL isimame sio kwa kubebwa bebwa kuweni na ubunifu.
Dk.Ndugulile amesema matumizi yao hayalingani na wanachokipata na kuwataka kuboresha huduma kwa wateja.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba alisema Shirika lake limeweza kujiendesha kwa faida kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kuanzia mwaka 2016/2017 kwa kutengeneza faida ya shilingi bilioni tano kwa mwaka tofauti na miaka mitano iliyopita kuanzia mwaka 2016 kurudi nyuma ambapo Shirika limekuwa likijiendesha kwa hasara.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Jim Yonazi aliwaeleza Mameneja hao kuwa watumie mbinu za kuongeza wateja na kutengeneza mazingira ya kukubalika katika maeneo wanayotoa huduma kama ilivyo kwa waganga wa tiba za asili na wahubiri wa dini ambapo wamejenga imani na wanatoa huduma kwa wafuasi wao
.