Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Ummy Mwalimu akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano na Wadau wanaojihusisha na shughuli za ukusanyaji , usafirishaji, uhifadhi na urejelezaji wa chuma chakavu uliofanyika katika ukumbi wa Mtana uliopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo akiongea wakati akimkaribisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Ummy Mwalimu kuongea na Wadau wanaojihusisha na shughuli za ukusanyaji , usafirishaji, uhifadhi na urejelezaji wa chuma chakavu katika ukumbi wa Mtana jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Wadau waliohudhuria Mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Ummy Mwalimu pamoja na Wadau wanaojihusisha na shughuli za ukusanyaji , usafirishaji, uhifadhi na urejelezaji wa chuma chakavu uliofanyika katika ukumbi wa Mtana jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka akiongea wakati wa Wadau wanaojihusisha na shughuli za ukusanyaji , usafirishaji, uhifadhi na urejelezaji wa chuma chakavu katika ukumbi wa Mtana uliopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
*****************************************************
Shughuli za Ukusanyaji, Usafirishaji, Uhifadhi na Urejelezaji wa Chuma Chakavu zinaweza kufanyika bila kuhatarisha Miundombinu ya Taifa na wakati huo huo kuchangia katika pato la Taifa. Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mh. Ummy Mwalimu kwenye Mkutano na Wadau wanaojihusisha na shughuli za ukusanyaji, usafirishaji, uhifadhi na urejelezaji wa chuma chakavu uliofanyika katika ukumbi wa Millenium Tower, jijini Dar es Salaam.
”Niwasihi sana kuhakikisha kuwa shughuli mnazizofanya haziwi chanzo cha uharibifu wa miundombinu yetu”, alisema Waziri Ummy.
Lengo la Mkutano huo ni kukuza uelewa wa Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Udhibiti na Usimamizi wa Taka Hatarishi) za mwaka 2019 na kujadili changamoto katika Utekelezaji na Usimamizi wa Kanuni hizo.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali imebaini kuwepo kwa hujuma ya miundombinu ya Taifa ikiwemo Reli, Barabara na majengo kutokana ongezeko la uhitaji wa vyuma chakavu kwa ajili ya malighafi za viwanda, jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa.
“Ninataka vyombo vya Ulinzi na Usalama kushiriki katika kuzuia hili. Kwa upande wa Ofisi ya Makamu wa Rais, tukibaini kuwa wenye vibali vya kukusanya, kusafirisha na kuhifadhi vyuma chakavu wanashiriki katika kuhujumu miundombinu vibali vyao vitafutwa”. alisema Waziri Ummy
Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali inathamini mchango wa Wadau katika shughuli za udhibiti na usimamizi wa taka hatarishi na kwa sasa dunia inaelekea kwenye uchumi wa mzunguko (circular economy), ambao unasisitiza kuwa “taka ni mali”, kwa hiyo ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za uhifadhi wa mazingira kwa maendeleo endelevu ni muhimu sana.
Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ina jukumu la kusimamia na kudhibiti taka hatarishi kama ilivyobainishwa kwenye vifungu 133-139 vya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.
Mkutano huo uliitishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira kwani aliona ni vyema kukutana na wadau wanaojihusisha na shughuli za ukusanyaji, usafirishaji, uhifadhi na urejelezaji wa chuma chakavu ili kwa pamoja kuweza kujadiliana namna bora ya kukabiliana na changamoto hizo na kutoa mapendekezo yatakayoimarisha usimamizi na udhibiti wa taka hatarishi kwa ujumla nchini.