Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akizungumza na Watendaji wa Wizara na Taasisi zake katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Maji Mhe.Juma Aweso amesitisha zoezi lililokuwa likiendelea kwa agizo la Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati(EWURA) la kuzitaka mamlaka za maji nchini kupandisha ankara za maji mpaka hapo atakapojiridhisha na kuruhusu utaratibu huo kuendelea.
Waziri Aweso ametoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili cha wizara ya maji na Taasisi zake ambapo amesema bado hajaridhika na kazi zinazofanywa na mamlaka hiyo katika eneo la udhibiti katika utoaji wa huduma za maji huku akiwataka kujipanga zaidi.
Awali Naibu Waziri wa Maji Mhe. Maryprisca Mahundi, amesema kuwa miradi mingi inayofanya kazi nchini imepitwa na wakati hivyo kuna haja ya kufanya taratibu na Mipango ya kuiboresha kutokana na uchakavu wa miundombinu na vifaa.
Mhe.Mahundi amewataka wataalam kufanya mapitio upya katika miradi hiyo nchi nzima na kuwasilisha taarifa ya namna ya kuikarabati na bajeti nzima itakayohusika kwa ajili ya maboresho.
Amesema kumekuwa na changamoto kubwa katika utekelezaji wa miradi ambayo imekamilika kutokana na jumuiya nyingi za maji kutofanya vizuri katika usimamizi mara baada ya kukabidhiwa miradi hiyo.
Amesema pia kumekuwa na changamoto ya miradi mingi kutokamilika ili hali akaunti za mameneja zina fedha, jambo hili linasababishwa na mameneja kutojiamini au kukosa kibali cha kutekelezeka majukumu yao kutoka kwa viongozi wa juu.
Kwa upande wake Naibu katibu mkuu wa wizara Maji, Nadhifa Kemikimba amesema hivi sasa kuna changamoto kubwa katika usimamizi wa vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kilimo, ufugaji na uchimbaji madini na shughuli nyingine zinazofanywa na binadamu.