*************************************************
Serikali imetoa vifaa na visaidizi maalum vya aina mbalimbali vyenye thamani ya Shilingi bilioni 3 kwa ajili ya wanafunzi 18,488, ambao wana mahitaji maalum wa shule za msingi na sekondari nchini ili kuwawezesha wanafunzi hao kumudu masomo katika shule zao.
Akizindua zoezi la usambazaji wa vifaa hivyo leo mjini Dodoma, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Selemani Jafo, amesema, Ofisi ya Rais – TAMISEMI kupitia Programu ya EP4R imeweza kununua jumla ya vifaa na visaidizi maalum 51,339 vya aina mbalimbali kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule za msingi na sekondari.
Amesema kuwa Vifaa hivi vilivyonunuliwa vimegharimu jumla ya Shilingi 2,833,374,280 na vitasambazwa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ambao wamegawanyika kwenye makundi maalum yapatayo manane.
Waziri Jafo ameyataja makundi hayo ya wanafunzi wenye mahitaji maalum kuwa ni Viziwi, Wasioona, Albino, Wenye Uoni Hafifu, Wenye Ulemavu wa Viungo, Wenye Ulemavu wa Akili, Wenye Usonji na Wenye Uziwi na kutokuona.
Amesema shabaha ya Serikali ni kuhakikisha watoto wote wa kitanzania wanapata elimu iliyokusudiwa ikiwa ni mpango wa utekelezaji wa sera ya Elimu ya mwaka 2014.
“Ofisi ya Rais TAMISEMI imeweka mkazo katika kukabiliana na vikwazo dhidi ya uwepo ushiriki na ujifunzaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum. Mojawapo ya hatua ambayo imechukua ni kununua vifaa maalum vya kielimu na visaidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum,” amesema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga, amesema, katika kipindi cha miaka mitano, 2016/2020 cha Serikali ya awamu ya Tano chini ya Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imefanya mambo mengi katika utoaji wa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ikiwemo kuongezeka kwa shule zinazo wahudumia wanafunzi wa Elimu ya Awali, zilizoongezeka kwa asilimia 46.1, msingi asilimia 23.9 na Sekondari 24.6.
“Mheshimiwa Waziri mbali na hayo, ongezeko la Watoto wenye mahitaji maalum walioandikishwa ni asilimia 46.1 kwa elimu ya awali, asilimia 34.0 kwa elimu ya msingi na asilimia 74.6 ni kwa sekondari,” alisema Nyamhanga.
Katibu Mkuu ameongeza kuwa, wanafunzi wenye Ulemavu wanaohitimu Elimu ya Msingi na kujiunga na Sekondari imeongezeka kutoka asilimia 69.9 mwaka 2016 hadi asilimia 76.3 mwaka 2020.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, anayeshughulikia Elimu maalum, Julius Migeha, alisema hivi sasa Serikali inaendelea na la kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum ili waweze kuandikishwa na kupatiwa elimu, hivyo akawataka wazazi wenye watoto wa aina hiyo kutoa ushirikiano kwa timu ili dhamira ya serikali iweze kutimia.
Katika mwaka wa fedha 2017/18, serikali ilifanikiwa kuendesha utaratibu wa kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum, ambapo jumla ya watoto 16,436 waliweza kufikiwa na kwa mwaka huu lengo la serikali ni kuwafikia Watoto 18,000.
Ofisi ya Rais TAMISEMI inajukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa utoaji wa elimu bora kwa wanafunzi wa Elimu ya Awali, Shule za Msingi na Shule za Sekondari, hii ni pamoja na kuhakikisha mahitaji muhimu ya kujifunzia na kufundishia yanapatikana kwa lengo la kupata idadi kubwa ya Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa letu bila kujali tofauti zao.