Mbunge wa Jimbo la Kibaha vijijini Michal Mwakamo kupitia tiketi ya Chama cha mapinduzi (CCM) akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari hawapo pichani kuhusina na mipango yake katika kuboresha sekta ya afya na kupambana na magonjwa ya mlipuko.(PICHA NA VICTOR MASANGU)
*************************************************
NA VICTOR MASANGU, PWANI
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Michael Mwakamo ameiasa jamii pamoja na kundi la mama lishe kuhakikishe kwamba wanazingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya ikiwemo suala zima la unawaji wa mikono kwa kutumia maji safi na salama yanayotiririka kwa kutumia sabuni ili kuepukana kabisa na wimbi la magonjwa ya milipuko ambayo ni hatari kwa afya za wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mikakati yake aliyojiwekea katika suala zima la kuboresha sekta ya afya Mwakamo alibainisha kwamba kwa sasa ameweka mikakati madhubuti ya kuweza kushirikiana na wataalamu wa afya kwa lengo la kutoa elimu na mafunzo juu ya umuhimu wa kunawa mikono hasa katika maeneo yenye mikusanyiko mingi ya watu.
“Mimi kama Mbunge wa jimbo la Kibaha mjini napenda kuchukua fursa hii kuwahimiza wananchi wangu wote pamoja na mama lishe kuweka mazingira ya kufanya usafi katika maeneo ambayo wanafanyia kazi lengo ikiwa ni kujilinda wao wenyewe pamoja na walaji kuondokana na magonjwa ya mlipuko,”alisema Mwakamo.
Pia Mbunge huyo aliongeza kuwa suala la uchafuzi wa mazingira ni hatari sana katika jamii ambayo inatuzunguka kwani linaweza kuleta madhara makubwa kwa baadhi ya wananchi kujikuta wanapata magonjwa hayo ya mlipuko ambayo chanzo chake kikubwa kinatokana na baadhi ya wananchi kutupa taka ovyo kitu ambacho sio kizuri kabisa kwa afya ya binadamu.
Pia aliipongeza serikali ya awamu ya tano pamoja na wataalamu mbali mbali wa masuala ya afya kwa kuelekeza nguvu zao kubwa katika kuhakikisha suala la usimamizi wa usafi wa mazingira linafanyiwa kazi kuanzia katika ngazi za chini hadi juu na kuwepa kuwapa fursa wananchi waweze kuendsha shughuli zao mbali mbali katika hali ya usafi.
Aidha Mwakamo alisema kuwa katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu yatano katika mpango wake wa kufanya usafi wa mazingira atahakikisha kwamba anashirikiana bega kwa began a wananchi wa jimbo lake la kuendesha zoezi la mara kwa mara katika maeneo ya makazi ya watu ili kuweza kusafisha mazingira yawe katika hali ya usafi.
“Kitu kikubwa mimi nitaweka utaratibu mzuri wa kuendelea kushirikiana na wananchi wa jimbo langu kuanzia ngazi za vijiji kuendesha zoezi la usafi wa mara kwa mara pamoja na kuchoma taka zote ambazo zinakuwa zimezagaa lengo ikiwa ni kufanya kuondokana kabisa na magonjwa ya milipuko ambayo yanaweza kujitokeza kama vile kuumwa na matumbo, kuhala pamoja na mengineyo,”alisisitiza Mwakamo.
Katika hatua nyingine aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kunywa maji safi na salama ambayo tayari yanakuwa yamechemshwa na kuuwa vijidudu ambayo vipo na kwamba itaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa kuendelea kujishughulisha katika kazi zao mbali mbali bila ya kuwa na changamoto ya kuumwa na magonjwa ya aina mbali mbali.