*************************************
Na Damian Kunambi, Njombe.
Kufuatia changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wa shule ya sekondari Mountain Livingston iliyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe wanafunzi wa shule hiyo wamemuomba Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kuwasaidia kutatua changamoto hizo ambazo ni uhaba wa walimu wa sayansi,ujenzi wa mabweni pamoja na kupata chakula shuleni hapo.
Ombi hilo wamelitoa baada ya mbunge huyo kutembelea shuleni hapo ambapo walimweleza kuwa Shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa bweni la wanafunzi wa kike huku wanafunzi wa kiume wakiwa hawana kabisa bweni kitu ambacho kinapelekea wanafunzi hao kwenda kuishi mitaani kitu ambacho kinapelekea wanafunzi hao kutosoma kwa utulivu.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake dada mkuu wa shule hiyo aliyetambulika kwa jina la Ester Kiowi amesema bweni lao ni chakavu sana pamoja na jiko la kupikia hivyo wanaiomba serikali kuwasaidia kukarabati ikiwemo na kuongeza mabweni mengine.
Naye mwanafunzi mwingine Hilary Mwankenja amesema mbali na uhaba huo wa mabweni pia wanaomba wawe wanapikiwa chakula shuleni hapo kwakuwa kwa sasa wamekuwa wakijipikia wenyewe kitu ambacho kinawapotezea muda wa kusoma.
Alisema kila jumamosi wamekuwa wakirejea majumbani kwao kwaajili ya kufuata vyakula na wanapokosa matokeo yake huingia mitaani na kudoko mazo yawatu yaliyopo mashambani.
“Natamani sana endapo tutapewa nafasi ya kupikiwa chakula hapa shuleni kwani kujipikia kumekuwa ni changamoto kubwa kwetu hivyo mbunge wetu tunaomba utusaidie kutatua changamoto hii”, Alisema Mwankenja.
Aidha kwa upande wa mbunge huyo amesema amezipokea changamoto zote na atazifanyia kazi kwa kushirikiana na mwenyekiti wa halmashauri hiyo Wise mgina ambaye alikuwa ni miongoni mwa msafara huo.
Amesema ni muhimu sana kwa wanafunzi kuwa na mabweni pamoja na kupata chakula shuleni huku akiwasii wanafunzi hao kuacha tabia ya kuiba mazao mbalimbali ya wananchi ikiwemo mihogo kwani kwa kufanya hivyo ni uvunjifu wa sheria za nchi.
“Wanafunzi ili waweze kusoma vizuri wanatakiwa kupata sehemu nzuri ya kulala pamoja na kupata chakula hivyo kutokana na changamoto mnayoipata inaweza kuwa ni moja ya sababu ya kutofanya vizuri katika masomo yenu”, Alisema Kamonga.
Sanjari na ahadi hiyo ya kutatua changamoto hizo pia mbunge huyo ameahidi kutoa kiasi cha shilingi laki mbili na nusu kwa kila division one itakayotoka shuleni hapo bila kujali idida ya alama hizo ambapo shilingi laki mbili ataikabidhi katika uongozi wa shule na shilingi elfu hamsini kwa mwalimo wa somo.
Pia amesema ili mwanafunzi aweze kuwa na afya bora na akili yenye kufikiri vyema tatakiwa kushiriki michezo mbalimbali hivyo ameahidi kupeleka jezi za wanafunzi wa kike na kiume pamoja na mipira kwaajili ya michezo mbalimbalia.
Baada ya kumaliza ziara shuleni hapo alienda katika kijiji cha Lupingu kilichopo katika kata ya Lupingu ambapo nako akakutana na changamoto mbalimbali ikiwemo wakazi wa eneo hilo kuomba kuongezewa kituo cha meli ya Mv. Mbeya ambapo wamependekeza kituo hicho kiwekwe Makonde ambapo mbunge huyu ameahidi kufikisha ombi hilo katika mahala husika.