…………………………………………………………………….
Na Muhidin Amri,Songea
CHAMA cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma,kimempongeza mkuu wa mkoa huo Christina Mndeme kwa kazi mzuri ya kusimamia ujenzi wa miundombinu ya barabara pamoja na kuunga mkono uamuzi wake wa kuhamisha kituo kikuu cha mabasi ya mikoani kutoka kituo cha zamani cha Mfaranyaki kwenda kituo kipya cha shule ya Tanga.
Hivi karibuni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme aliwataka wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani na yale yanayofanya safari ndani ya mkoa kuanza kutumia kituo kipya cha mabasi shule ya Tanga ambacho ujenzi wake umekamilika tangu mwaka jana.
Hayo yamesemwa jana na Mwenyekiti wa Chama hicho mkoahi hapa Oddo Mwisho wakati akizungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika jana mjini Songea.
Mwisho alisema, hatua ya kuhamisha kituo kikuu cha mabasi kutoka eneo la Mfaranyaki kwenda kata ya Shule ya Tanga ni uamuzi sahihi kwani licha ya ukweli kwamba utapanua mji wa Songea pia Manispaa ya Songea itaongeza wigo wa kukusanya mapato yake.
Alisema, kituo cha mabasi Shule ya Tanga kimeigharimu serikali zaidi ya shilingi bilioni 6 hadi kukamilika kwake,kwa hiyo uamuzi wa Mkuu wa mkoa ni sahihi kwa kuwa utasaidia kuendeleza Manispaa ya Songea katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi na biashara hasa ikizingatia kuwa fedha zilizotumika katika ujenzi huo ni mkopo.
Amewataka wananchi wa Songea kukubali uamuzi huo kwani una faida nyingi sio kwa serikali tu bali hata kwa jamii kwani sasa wataweza kukitumia kituo hicho kufanya biashara mbalimbali kwa kujenga majengo ya biashara jirani na kituo hicho na wenyeji kuuza ardhi yao kwa bei kubwa.
Aidha,amewapongeza madiwani wa Manispaa hiyo wakiongozwa na Mstahiki Meya Michael Mbano kwa kwa kukubali uamuzi ya mkuu wa mkoa na kuwataka kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inafanya kazi na kutoa huduma kwa wananchi.
Alisema, Chama cha Mapinduzi kitahakikisha kinakuwa bega kwa bega na watumishi wa serikali katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo na kusisitiza kuwa ni wajibu wao kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.
Pia, amelipongeza Jeshi la Polisi mkoa wa Ruvuma kwa kusimamia vyema matumizi ya kituo kipya cha mabasi na kulitaka kuchukua hatua kali kwa madereva na watakaokahidi kutumia kituo hicho.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Tina Sekambo alisema, kwa sasa mapato yanayokusanywa katika kituo kipya cha mabasi Shule ya Tanga yameongezeka kutoka wastani wa shilingi 450,000 hadi kufikiwa shilingi 907,000.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani humo kuwakamata na kuwachukulia hatua kali madereva wa malori wanaomwaga makaa ya mawe barabarani.
Mndeme ameziagiza Halmashauri nane katika mkoa huo kutunga sheria ambazo zitawabana madereva hao na watu wengine wanaochafua mazingira na kuharibu miundombinu ya barabara zinazojengwa kwa gharama kubwa na serikali.
Alisema, madereva wanaofanya vitendo hivyo sio wanachafua mazingira tu bali hata kupunguza mapato ya Serikali kwani wanapofikisha kiwandani kwa ajili ya matumizi, uzito unapungua na hivyo kushindwa kupata uzito unaopaswa kulipiwa kodi sahihi.
Aidha ameliagiza jeshi hilo kushirikiana na wakala wa barabara Tanroad kuwasaka watu walioiba moja ya kioo cha cha kinachoonyesha usalama(safety Millor) kwenye kona kali eneo la Luhekei kwenye barabara kuu ya Mbinga Mbambabay inayejengwa na kampuni ya Chico.
“ni ajabu sana kabla ya barabara haijafunguliwa watu wameiba moja ya alama zilizowekwa,hatuwezi kuishi na wezi katika mkoa wetu,polisi na Tanroad hakikisheni mnawatafuta watu hao na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Katika hatua nyingine Mndeme ameiagiza wakala wa barabara mjini na vijijini Tarura mkoa wa Ruvuma kuongeza mtandao wa barabara za lami katika makao makuu ya Halmashauri na wilaya na kufunga taa katika makutano ya Mahenge na Mwembachai katika Manispa ya Songea ili kusaidia usalama wa vyombo vya moto na watembea kwa miguu katika maeneo hayo.