********************************************
11 Januari, 2021 – Dodoma
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) inawahakikishia wananchi kuwa hali ya upatikanaji wa mafuta ya kula itatengemaa mara baada ya kuanza upakuaji wa mafuta ya kula yanayoingizwa kutoka nje ya nchi kupitia bandari yetu ya Dar es salaam.
Changamoto ya uhaba wa mafuta ya kula umetokana na upungufu wa uzalishaji na kutegemea uagizaji wa mafuta ya kula nje ya nchi, bei ya mafuta ya kula hutegemea soko la bidhaa hiyo kulingana na msimu na mabadiliko ya bei ya bidhaa hiyo katika soko la Dunia.
Serikali imezipatia leseni kampuni mbili za uagizaji wa mafuta ya kula ambazo ni East Coast Oil and Fats Ltd na Murzah Wilmar East Africa Ltd. Kampuni hizo zimekuwa zikiingiza mafuta ya kula nchini ili kukidhi upungufu wa tani 365,000 MT kwa mwaka ya mahitaji halisi ya mafuta hayo ya tani 570,000 MT kwa mwaka wakati kiasi kinachozalishwa nchini ni tani 205,000 MT kwa mwaka (TARI-2020).
Aidha, meli mbili zimeingia bandari ya Dar es salaam. Meli aina ya UACC SHMIYA iliyowasili Bandari ya Dar es Salaam tarehe 10 Desemba, 2020 ambayo ilipangwa kushusha shehena tarehe 11 Januari, 2021, iliruhusiwa kuanza kushusha shehena husika kuanzia tarehe 30 Desemba, 2020 na kukamilisha ushushaji tarehe 03 Januari, 2021. Kiasi cha mafuta ya kula yenye ujazo wa 21,800 MT kimepakuliwa katika meli hiyo na sasa kiko tayari kuingia sokoni. Aidha, meli nyingine iitwayo MELATI SATU ya shehena ya mafuta ya kula ya ujazo wa 26,450 MT imetia nanga alfajiri ya tarehe 5 Januari, 2021 katika Bandari ya Dar es Salaam na ratiba ya ushushaji wa shehena inaonesha kuwa ni tarehe 19 Januari, 2021 hadi tarehe 22 Januari, 2021.
Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inaharakisha ushushaji wa mafuta ya kula yanayoingia kutoka nje ya nchi kupitia bandari ya Dar es salaam ili kuharakisha upatikanaji wa mafuta kwa wananchi na kupunguza kupanda kwa bei.
Pamoja na hayo Wizara imewekeza nguvu katika Mkoa wa Kigoma kupitia agizo la Waziri Mkuu kuhusu ushiriki wa Taasisi za Umma katika uzalishaji wa mchikichi kwa ajili ya usindikaji wa mafuta ya kula. Taasisi hizi ni pamoja na Jeshi la Magereza Tanzania, Taasisi ya utafiti wa Kilimo (TARI), na Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo na Biashara ndogo (SIDO).
Vilevile, Serikali imeendelea kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vikubwa, vya kati na viwanda vidogo vya kusindika mbegu za mafuta ili kutatua tatizo la uhaba wa mafuta ya kula nchini.