MIAKA 57 YA MAPINDUZI MATUKUFU YA ZANZIBAR
(Na Jovina Bujulu – MAELEZO)
“ Mapinduzi ya Zanzibar yana thamani kubwa kwa sababu ndiyo yaliyokata minyororo ya ubaguzi na aina zote za dhuluma zilizokuwa zinawakabili Wafanyakazi na Wakulima wa Zanzibar”. Hayo ni maneno yaliyowahi kutamkwa na Rais wa Awamu ya saba wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein katika mojawapo ya maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo husherehekewa kila ifikapo tarehe tarehe, 12, Januari.
Mapinduzi ya Zanzibar yalifanyika tarehe 12, Januari, 1964 ambapo mwaka huu yanafikisha miaka 57, huku Visiwa hivyo vikishuhudia maendeleo makubwa ya kiuchumi na kuimarika kwa ustawi wa wananchi wake.
Haya ndiyo Mapinduzi yaliyoikomboa Zanzibar na watu wake na kuleta Uhuru wa kweli kwa wananchi wote wa Zanzibar na kufungua ukurasa mpya wa maendeleo katika Visiwa hivyo na watu wake.
Waasisi wa Mapinduzi pamoja ni Hayati Mzee Abeid Amani Karume pamoja na viongozi wenzake ambao walijitoa mhanga kwa ajili ya kuikomboa Zanzibar dhidi ya dhuluma, manyanyaso na ubaguzi kwa wananchi wa Visiwa hivyo.
Katika kipindi cha miaka 57 ya Mapinduzi hayo mafanikio mengi yamepatikana hasa kutokana na kuendelea kuwepo kwa amani, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wote wa Zanzibar.
Katika hotuba iliyotolewa wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi hayo na aliyekuwa Rais wa Awamu ya saba wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein aliwahimiza wananchi wa Zanzibar kuisimamia amani iliyopo na kufuata misingi ya sheria ikiwa ni ishara ya kuyaenzi na kuyadumisha Mapinduzi hayo.
Aidha, Dkt. Shein alibainisha kuwa ustawi wa wananchi wa Zanzibar umezidi kuimarika kutokana na kuongezeka kwa Pato Halisi la Taifa kwa mara 1.6 zaidi kutoka thamani ya shilingi bilioni 1,768 mwaka 2010 hadi kufikia thamani ya shilingi bilioni 2,874 mwaka 2018.
Akiwasilisha Mpango wa Maendeleo na bajeti 2020/21 na 2022/23, aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar katika Serikali ya Awamu ya saba, , Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa alisema kuwa uchumi wa visiwa hivyo unakua kwa asilimia saba huku pato la mwananchi likiongezeka kutoka shilingi 942,000 mwaka 2010 hadi kufikia shilingi 2,323,000 mwaka 2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 147.
Kukua kwa uchumi Visiwani Zanzibar kumepelekea kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato mwaka hadi mwaka. Hali hii ya kukua kwa uchumi inakwenda sambamba na kuimarika kwa huduma za jamii kama vile upatikanaji wa nishati katika maeneo mengi, huduma ya maji, ongezeko la shule, dawa katika hospitali na uboreshaji wa miundombinu.
Zanzibar pia imeendeleza jitihada katika suala la uwekezaji ambapo miaka tisa iliyopita Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), imeweza kuwavutia wawekezaji katika miradi mbalimbali ambapo hadi kufikia mwaka 2018 jumla ya miradi 304 ilitekelezwa na kuzalisha ajira 16,866.
Aidha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imeendelea kuhamasisha wawekezaji wazalendo ili waweze kuanzisha viwanda kwa lengo la kuhakikisha bidhaa nyingi zinazalishwa visiwani humo na kuongeza usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi kwa kutambua uchumi wa viwanda ndio uchumi imara zaidi na himilivu.
Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya viwanda SMZ ilianzisha Wakala wa Kusimamia na Kuendeleza Viwanda Vidogo vidogo na vya Kati (SMIDA) pamoja na kupitisha sera mpya ya viwanda ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa ujumla.
Baadhi ya viwanda vilivyoko Visiwani humo ni pamoja na Turky Mifuko kinachotengeneza mifuko, kiwanda cha Zanto kinachosarifu tungure na pilipili, kiwanda cha Messab Packaging ambaco kinazalisha vifungashio, kiwanda cha kusarifu zao la chumvi, kiwanda cha kuzalisha mafuta ya nazi, kiwanda cha kutengeneza mabati na kiwanda cha kusarifu korosho.
Kwa upande wa elimu, Zanzibar imepiga hatua kubwa kwa kutoa elimu bure ikiwa ni utekelezaji wa malengo ya Mapinduzi ya kutoa elimu bure bila ubaguzi kama ilivyotangazwa na Hayati Mzee Abeid Amani Karume, tarehe 23, Septemba, 1964. Kabla ya Mapinduzi elimu Visiwani humo ilikuwa inatolewa kwa malipo na kwa matabaka.
Kwa sasa miundombinu ya elimu Zanzibar imeimarika kwa kiwango kikubwa katika ngazi zote. Idadi ya shule za maandalizi imeongezeka kutoka 242 mwaka 2011 hadi kufikia 368 mwaka 2020, ambapo idadi ya wanafunzi wa ngazi ya elimu ya maandalizi imeongezeka kutoka wanafunzi 33,229 mwaka 2011 na kufikia wanafunzi 92,098.
Aidha, ngazi ya elimu ya msingi idadi ya shule imeongezeka kutoka 200 mwaka 2011 zikiwa na wanafunzi 237,690 na kufikia shule 431 mwaka 2020 zikiwa na wanafunzi 313,097. Katika ngazi ya sekondari , uandikishaji wa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne umeongezeka kutoka 77,671 mwaka 2011 na kufikia wanafunzi 124,493 mwaka 2020. Ongezeko la shule na wanafunzi linakwenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya shule na ujenzi wa sekondari za kisasa zenye majengo ya ghorofa.
Pia kumekuwepo utoaji wa mafunzo ya Amali yanayotolewa kwa wanafunzi kulingana na mahitaji ya soko la ajira. Programu hii inawawezesha vijana kujiajiri ili kujikwamua na umaskini.
Kwa upande wa Afya, SMZ imefanikiwa kuimarisha huduma za afya kuanzia ngazi ya familia ambapo imepiga hatua kubwa katika kusambaza huduma za afya sehemu mbalimbali na kuwafikia wananchi walio wengiikiwa ni pamoja na kuimarisha hospitali ya Mnazi Mmoja kufikia hatua ya kuwa ya rufaa na moja ya hospitali zinazotoa mafunzo katika ukanda wa Afrika Mashariki. Aidha SMZ imefanikiwa kuongeza madaktari bingwa na wafanyakazi wa kada nyingine za afya, kuongeza vitendea kazi muhimu ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na kuongeza vituo vya afya.
Mafanikio mengine yanaonekana katika upatikanaji maji safi na salama ambapo SMZ kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), imefanikisha upatikanaji wa maji kwa asilimia 83 kwa mwaka 2020, ambapo mradi wa matenki makubwa ya kuhifadhi maji wenye kuzalisha lita milioni 37.7 za maji umeongeza upatikanaji wa maji. Maboresho mengine ni pamoja na ukarabati na uchimbaji wa visima ikiwa ni pamoja na kuviwekea mitambo ya kusukuma maji.
Rais wa Awamu ya Nane wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi akizindua kwa mara ya kwanza Baraza la 10 la Wawakilishi baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka 2020, alisema kuwa viongozi waliomtangulia wamefanya kazi kubwa ya kuitoa Zanzibar ilipokuwa na kuifikisha hapo na kwamba jukumu lake sasa ni kuendeleza mazuri yaliyoachwa na Rais aliyemtangulia Dkt. Ali Mohamed Shein na kuipeleka nchi mbele ikiwa ni pamoja na kutafsiri upya Mapinduzi na Muungano katika kizazi kipya.
Akisisitiza kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Mwinyi alisema, “ Lengo la Mapinduzi si tu kuondoa usultani, bali ni kuleta uhuru na ustawi kwa wananchi wa Zanzibar, ni matamanio yangu kuyadumisha Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuyatafsiri katika muktadha na mahitaji ya sasa ambayo ni ukombozi wa kiuchumi, kaulimbiu ya Mapinduzi hayo ndiyo tafsiri ya Serikali nitakayoiunda”.
Aidha, aliahidi kuendeleza ustawi wa wananchi kwa kuimarisha mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi ili uongeze uwezo wa kutoa huduma zilizo bora kwa wananchi walio wengi, kusajili wajasiriamali na kuwapatia vitambulisho, kuwa na mfumo bora wa kulipa kodi mara moja kwa mwaka pamoja na kutoa mafunzo kwa wajasiriamali. Aliongeza kuwa SMZ itaendelea kuwatunza wazee kwa kuwapatia chakula bora, matibabu na kuendelea kutoa pensheni jamii kwao.
Mwaka huu, Zanzibar inasherekea miaka 57 tangu kufanyika kwa Mapinduzi visiwani humo huku Awamu zote za utawala zikifanya kazi chini ya misingi ya Mapinduzi hayo ambayo ni pamoja na kuwaendeleza wananchi kiuchumi, kisiasa na kijamii.
MWISHO