MCHAMBUZI wa masuala ya Kisiasa na Jamii mkoani Iringa, Mugabe Kihongosi ameishauri serikali kuanzisha shule maalum kwa ajili ya walemavu tu tofauti na shule nyingi za sasa zikiwa mchanganyiko.
Kihongosi ambaye alikuwa mgombea nafasi ya Ubunge Jimbo la Kilolo katika kura za maoni alisema kuwa walemavu wanatakiwa kupewa kipaumbele kama ambavyo Rais John Magufuli amejidadavua kuwasaidia katika kipindi hiki Cha uongozi wake.
Alisema kuwa endapo zitaanzishwa shule maalum za walemavu zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupata wasomi walemavu na kurahisisha zaidi mahitaji yao hasa ya kimiundo mbinu ambapo baadhi ya shule mchanganyiko inakosekana.
Aidha ametoa wito kwa taasisi mbali mbali binafsi kuhakikisha kuwa zinaweka wakalimani wa lugha za alama kwenye maeneo ya kazi kwa lengo la kuwasaidia watu wenye changamoto ya ya uziwi wapate kusikilizwa na kuhudumiwa vizuri
Alisema kuwa taasisi nyingi nchini hazina huduma ya wakalimani hali ambayo inawapa wakati mgumu viziwi katika kupata huduma kwani maelewano yanakuwa hakuna hivyo ni jukumu la kila taasisi kuweka wakalimani ili wapate huduma kama ilivyo kwa watu wasiona ulemavu wa kusikia.
Kihongosi alisema kuwa Walezi waishio na watu wenye ulemavu wa kusikia(viziwi) kutowanyanyapaa badala yake wawape haki zote za msingi wanazostahili kama wanazopata watu wasioa na ulemavu ikiwemo elimu.
Aidha alitoa wito kwa jeshi la polisi kutambua kuwa katika jamii kuna walemavu wa kutosikia hivyo wakati wa kufanya kazi zao wasikamate ovyo watu na kuwapiga pasipokujua yupo katika kundi lipi.
Aliongeza kuwa walezi na wazazi wenye watoto walemavu wasiwafiche ndani kwani Wana haki sawa za kupata elimu Kama ambavyo watoto wengine wanapata
Alisema ifike wakati serikali iweke adhabu Kali kwa wazazi au walezi wanaowaficha watoto ndani kwani ni kukiuka misingi ya kibinadamu ya kupata elimu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Walemavu, Philemon Kisinini alisema kuwa moja ya changamoto ambazo walemavu wenye matatizo ya uziwi wamekuwa wakikumbana nazo kuwa ni pamoja na wanapokuwa hospital, polisi, kwenye nyumba za ibada imekuwa vigumu kwao kusikilizwa .
Alitoa wito kwa kuiomba serikali kuwawekea wakalimani wa lugha za alama yao ili nao wapate kusikilizwa shida zao na kutekelezewa kama ilivyo kwa watu ambao hawana Matatizo hayo