Waziri wa Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akiongea na Viongozi wa Vyama,Bodi na Mabaraza ya kitaaluma vilivyopo chini ya sekta ya afya nchini
Naibu Waziri Dkt. Godwin Mollel akiongea wakati wa kikao kazi na mabaraza,bodi na vyama vya kitaaluma kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa
Baadhi wa watendaji wa wizara ya afya makao makuu wakifuatilia mkutano huo ambao unajadili maadili na weledi wa wanataaluma kwenye vituo vya vya kutolea huduma nchini
Washiriki wa kikao kazi hicho kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa
*********************************************
Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma
Vyama, Mabaraza pamoja na bodi za kitaaluma nchini vimetakiwa kudhibiti maadili na weledi katika utendaji kwa watumishi wa sekta ya afya nchini ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa kikao na viongozi hao kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijiji Dodoma.
Dkt.Gwajima amesema kuwa vyama, bodi na mabaraza ya kitaaluma ndio wasimamizi wakuu na wadhibiti wa maadili na weledi ambapo wananchi bado wanakutana na changamoto nyingi za maadili na weledi wakati wa upataji huduma za afya.
“Kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya uchaguzi kurasa 137 imeandikwa kushirikiana na vyama vya kitaaluma vya kada ya afya katika kusimamia uzingatiaji wa maadili na weledi katika utendaji wa watumishi hilo ndio tunalotekeleza. “Amesisitiza Dkt. Gwajima.
Amesema wanapofanya ziara kwenye mikoa mbalimbali wanakutana na kero zitokanazo na kufifia kwa maadili na weledi wa utendaji, huku akiweka wazi kuwa, haya yote yanadhibitiwa na vyama, bodi na mabaraza ya kitaaluma.
“Ili tuweze kuhuisha hayo yote, lazima tukae pamoja na kuangalia mifumo yao ya utendaji kazi ukoje hadi unatoa mianya ya baadhi ya wanataaluma kukosa maadili na kuleta malalamiko mengi kutoka kwa wananchi?,Aliuliza Dkt. Gwajima
Aidha, Dkt. Gwajima amesema kutokana na malalamiko hayo inafanya kuonekana kukosa meno ya vyama hivyo vya kitaaluma, hivyo kikao hicho kikubwa ni kuambina ukweli na kuwakumbusha majukumu yao na wafahamu kuna tatizo kwa wanataaluma wao ndio mana hawashtuki na hata wengine kuvunja maadili bila kujali kama kuna mabaraza ya kitaaluma na kubadilika ili kuondoa kero kwa wananchi.
Kwa upande wa kuwa na mwamvuli mmoja wa mabaraza yote ni kwamba itasaidia kuwa na timu moja na matumizi ya fedha ya kuendesha mabaraza yote yatapungua na kuongeza ufanisi na tija ya wataalam wengine ili wakae kwenye maadili.
Naye Naibu Waziri Dkt. Godwin Mollel amewataka viongozi hao kuwajibika ili kuondoa matatizo ambayo ama wao kama mabaraza hawayaoni au yanaonwa na viongozi wa wilaya eneo husika.
Dkt. Mollel aliendelea kusema kuwa, wataalamu wengi hivi sasa hawafanyi kazi kwa kuzingatia maadili na hivyo kusababisha makosa mengi ya kitaaluma yanafanyika kwenye vituo vya kutolea huduma na wananchi wengi kupoteza maisha na wengine kupata athari kwenye jamii.
“Tunakuta makosa kwenye taaluma mfano dawa zinaibiwa lakini wewe mwenye baraza lako na unasimamia maadili hulioni hili hivi hujioni kwamba na wewe unatakiwa kuadhibiwa? Aliuliza Dkt.Mollel
Hatahivyo amewataka viongozi hao kujitafakari kama wanatosha kwenye mabaraza yao kama wanashindwa wao kugundua matatizo yaliyopo chini kwani wanakuwa wameshindwa kusimamia na kufanya kazi zao vizuri kwa kutoa adhabu kwa wanaofanya makosa na kusababisha matatizo kwa wananchi.