Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Hati ya Ardhi aliyekuwa Waziri wa Ujenzi ambaye sasa ni Mbunge wa Jimbo la Katavi Isack Kamwelwe akiwa katika ziara yake ya kikazi kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Tanga tarehe 7 Januari 2021. Kushoto ni Meya wa Jiji la Tanga Abdulrahman Shiloow.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela (Kushoto) na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi ambaye sasa ni Mbunge wa Katavi Isack Kamwelwe alipowasili kwa ziara ya siku moja katika mkoa wa Tanga kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi tarehe 7 Januari 2021. Wa pili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kabla ya kuzungumza na watendaji wa sekta ya ardhi kwenye mkoa huo na kugawa hati za ardhi kwa wakazi wa jiji la Tanga akiwa katika ziara yake ya kikazi tarehe 7 Januari 2021. Aliye kaa mbele ni Mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shigela.
…………………………………………………………………….
Na Munir Shemweta, WANMM TANGA
Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula amewataka watendaji wa sekta ya ardhi nchini kufanya utafiti sababu zinazowafanya wamiliki wa ardhi kushindwa kujitokeza kuchukua hati za ardhi zilizokamilika.
Dkt Mabula alitoa kauli hiyo leo tarehe 7 Januari 2021 katika ukumbi wa Halmashauri ya jiji la Tanga wakati akigawa Hati za Ardhi kwa wakazi wa Jiji hilo akiwa katika ziara yake ya siku moja katika mkoa huo kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.
Dkt Mabula alisema, ni lazima watendaji wa sekta ya ardhi nchini kuanza kujiuliza tatizo liko wapi mpaka wamiliki wa ardhi ambao hati zao zimekamilika wanashindwa kujitokeza kuzichukua hati zao katika ofisi za Wasajili wa Hati Wasaidizi kwenye Ofisi za Ardhi za Mikoa.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mabula, kati ya wamiliki wa ardhi 80 waliotaarifiwa kwenda kuchukua hati zao zilizokamilika katika Halmashauri ya jiji la Tanga ni wamiliki 8 tu waliojitokeza kuzichukua jambo alilolieleza kuwa siyo sahihi.
Aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi kuwahimiza wamiliki wa ardhi wakati wa kuandaliwa hati kwenda kuchukua hati kwa wakati sambamba na kuwakumbusha masharti ya umiliki kama vile viwango wanavyotakiwa kulipa kama kodi ya pango la ardhi pamoja na kuendeleza kiwanja ndani ya miaka 3.
“Ukichukua Hati unaongeza thamani ya eneo lako maana usipochukua kunakuwa na masharti mengi wakati wa kutaka kuuza, eneo la milioni 20 unaweza kuliuza kwa milioni 5 huku anayelinunua anaweza kuliuza hata kwa milioni 200 ” alisema Dkt Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula aliongeza kwa kusema, kwa sasa Watendaji wa Wizara yake wanafanya kazi kama mchwa ili kuhakikisha mambo wanayopanga yanafanyika kwa mafanikio makubwa.
Mmoja wa wananchi waliopatiwa Hati na Naibu Waziri Dkt Mabula mkoani Tanga ni aliyekuwa Waziri wa Ujenzi ambaye sasa ni Mbunge wa Jimbo la Katavi Mhandisi Isack Kamwele ambaye aliipongeza Wizara ya Ardhi kwa utaratibu iliyouanzisha ya kuwapigia simu wamiliki wa ardhi ambao hati zao zimekamilika.
“Mimi nilipigiwa simu na ofisi ya Ardhi mkoa kuelezwa kuwa hati yangu iko tayari, uamuzi wa kupigiwa simu ni utaratibu mzuri na hii sasa ni dunia ya kwanza na tukiendelea na utaratibu huu basi malalamiko yatapungua sana ila naomba muongeze kasi katika utoaji vibali vya ujenzi” Alisema Mhandisi Kamwele.