Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhandisi Martine Ntemo wa mwisho kushoto akizungumza na baadhi ya watendaji wa halmashauri wa mji Kibaha wakati alipofanya ziara yake ya kikazi kwa ajili ya kutembelea miradi mbali mbali ya maendeleo ili kuweza kubaini changamoto zilizopo ili kuzitafutia ufumbuzi.
************************************************
NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
MKUU wa Wilaya ya Kibaha . Mhandisi Martine Ntemo ametoa agizo kwa watendaji wa kata kuhakikisha wanasimamia uundaji wa vikundi vya usafi kwenye maeneo yao.
Akiongea na waandishi wa habari Mjini Kibaha Ntemo alisema vikundi hivyo ndivyo vinavyosaidia kuimarisha usafi kwenye maeneo yao na kuepukana magonjwa ya mlipuko.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kila mtendaji anatakiwa kuhakikisha vikundi hivyo vya uzoaji taka vipo kwenye maeneo yao na vinafanya kazi.
Alisema viongozi wa shule pia wanatakiwa kuzingatia usafi wa mazingira hususani kipindi hiki cha mvua na msimu wa maembe unaoendelea .
Naye Mkurugenzi wa mji wa Kibaha Jenifa Omolo akizungumzia kuhusiana na suala la vyoo kwa kaya ambazo hazina alisema ipo kampeni inaendelea kuhakikisha kila nyumba ina choo.
Omolo alisema wapo Maofisa afya ambao wanaendelea na kampeni ya kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora lengo kuwaepusha wananchi na magonjwa ya mlipuko.
Hivi karibuni mwenyekiti wa mtaa wa Tangini Shauri Yombayomba alisema zipo baadhi ya kaya katika mtaa wake bado hazina vyoo huku kaya nyingine zikikabiliwa na uhaba wa vyoo kutokana na idadi kubwa ya watu.