***********************************************
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa na vitendo vya baadhi ya wananchi kuwatumia Watu Wenye Ulemavu kwa kuwafanya ombaomba mitaani kwa lengo la kujiingizia kipato. Aidha, wamekuwa wakiwafanyia vitendo vingine vingi vya udhalilishaji. Vitendo hivyo ni kinyume na haki za binadamu zilizoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 ambazo zinasisitiza utu wa mtu kuheshimiwa.
Tume inaungana na Serikali pamoja na wadau wote nchini kukemea vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji dhidi ya Watu Wenye Ulemavu na inatoa rai kwamba vitendo hivi vikomeshwe mara moja na wahusika wote wachukuliwe hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Tume inaishauri Serikali kuendeleza juhudi zake za kuwatambua Watu Wenye Ulemavu na mahitaji yao ili kuwawekea mazingira mazuri kupitia mfumo wa uwezeshaji ili waweze kujitegemea. Aidha, Serikali iendelee kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ili kubaini vitendo vya udhalilishaji dhidi ya Watu Wenye Ulemavu.
Tume inawasihi wananchi kutoa taarifa katika mamlaka husika kuhusu vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji dhidi ya Watu Wenye Ulemavu vinavyofanyika katika maeneo yao.
Pia, Tume inawataka Wananchi kuachana na imani, mila, desturi na mitazamo potofu ambavyo huwafanya Watu Wenye Ulemavu kujiona hawakubaliki, hawawezi chochote, na hawana mchango wowote kwa jamii inayowazunguka na Taifa kwa ujumla katika shughuli zinazohusu maendeleo.
Vile vile, Tume inawaomba wadau wote kuungana pamoja kutoa elimu kwa jamii na kupinga vitendo vyote vya udhalilishaji na unyanyasaji dhidi ya Watu Wenye Ulemavu.
Mwisho, Tume itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinalindwa, zinakuzwa na kutetewa nchini.