********************************************
CHUO cha Furahika Education College kilichopo Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam kimeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Joseph Magufuli katika kuleta maendeleo kwa kutoa mafunzo ya ufundi bure kwa mabinti na vijana waliokatiza masomo yao kutokana na sababu mbalimbali na katika kipindi hiki ambacho shule zinafungua uongozi umewataka wazazi kuwapa vijana nafasi ya kupata elimu hiyo ili waweze kujikomboa kiuchumi.
Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Chuo hicho tawi la Dar es Salaam David Msuya amesema kuwa, katika kuhakikisha uchumi wa Taifa unakuwa zaidi Chuo hicho kimetoa nafasi 5 katika Halmashauri za Kibaha vijijini, Bagamoyo na Kisarawe kutoa vijana wakike watakaojiunga na Chuo hicho ikiwa ni sehemu ya kukuza elimu na kuwanufaisha vijana wengi zaidi.
“Changamoto katika sekta ya elimu bado ipo, wazazi bado wazito katika kuwahimiza na kuwaleta vijana kupata elimu…sisi hatuchukui ada ni vifaa vya kujifunzia pekee ndivyo wazazi huchangia.” Amesema.
Aidha amesema, chuo kimefunguliwa Januari nne na wametoa siku saba zaidi ili wazazi waweze waweze kuwaleta vijana kupata elimu na ujuzi utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi.
Aidha amewaomba maafisa maendeleo ya jamii pamoja na Taasisi za dini yakiwemo makanisa na misikiti kuwapeleka chuoni vijana wenye uhitaji ili waweze kupata elimu bure.
Kuhusiana na mradi wa zao la parachichi wanaousimamia kwa ufadhili wa shilingi milioni 600 kutoka Canada, Msuya amesema zao hilo ni muhimu na lenye tija ulimwenguni na hadi sasa shilingi milioni 400 zimetolewa kwa wakulima wanaolima zao hilo kutoka Mkuranga, Bagamoyo na Kisarawe.
Pia ametumia wasaa huo kuipongeza Serikali kwa juhudi zinazofanyika katika kukuza uchumi wa Taifa na kuiomba kuangalia suala la upigwaji wa viboko kwa watuhumiwa kunakofanywa na viongozi mbalimbali wa Serikali na kueleza kuwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu kinachotakiwa ni kufuata mkondo wa sheria.
Kuhusiana na mafunzo yanayotolewa chuoni hapo msuya amesema wanatoa kozi za ufundi kushona, elimu ya Kompyuta, mafunzo ya hoteli, upambaji, mitindo na ususi.
Pia kozi nyingine zinazotolewa chuoni hapo ni pamoja na Muziki, ufundi ujenzi, uchomeleaji, ufundi wa magari, kilimo, ufundi wa mabomba na ufugaji.