**********************************************
Na MWAMVUA MWINYI, Pwani
Jan 6
MBUNGE wa Jimbo la Mafia ,Mkoa wa Pwani Omary Kipanga, ametoa rai kwa wakazi jimboni humo kusaidia kwa hali na mali sekta ya michezo ili kuendeleza vipaji vya vijana na kuitangaza Mafia.
Aidha amewaomba kuiombea timu ya Black Rhino ya jimboni humo inayoshiriki Ligi ngazi Mkoa ili iweze kufuzu.
Kipanga ambae ni Naibu Waziri wa Elimu alitoa rai hiyo wakati akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa, ambapo alisema sekta hiyo yenye wapenzi wengi wa masuala ya michezo inahitaji msukumo na msaada mkubwa ili kuviwezesha vipaji vilivyopo viweze kuibuliwa.
Alisema kuwa Mafia kuna vijana wenye uwezo mkubwa wa kushiriki michezo mbalimbali hususani soka, hivyo ni wajibu wao kuiangalia sekta hiyo kwa jicho la tatu litalowasaidia kusukuma mbele zaidi vipaji hivyo.
“Katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inasisitiza sekta ya michezo, hivyo basi nitumie fursa hii kwa wana-Mafia waliopo jimboni na nje ya Jimbo kujitokeza kusaidia vilabu vyetu, ili viweze kusonga mbele ukizingatia sekta hiyo ina mchngo mkubwa kwenye upatikanaji wa ajira,” alisema Kipanga.
Akizungunzia ushiriki wa timu ya Black Rhino ya jimboni humo inayoshiriki Ligi ngazi Mkoa kuanzia hatua ya makundi mpaka sasa tisa bora, Naibu Waziri huyo alisema kuwa anaimani kwamba watafanya vizuri katika hatua hiyo.
“Mimi na viongozi wenzangu wa chama na serikali tumeshiriki kuwaaga vijana wetu ambapo wamesafiri kwenda Bagamoyo tayari kwa hatua ya tisa bora iliyoanza Jan 3 uwanja wa Mwanakalenge wilayani humo, imani yetu wana-Mafia ni kwamba watafanya vizuri” alisema Kipanga