MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge ,akitoa maelekezo kwa Mkandarasi anayejenga kipande cha barabara ya Nghambi wilayani Mpwapwa baada ya leo 5.1.2021 kufanya ziara ya kukagua maeneo yaliyoathiriwa na Mvua.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa kipande cha barabara ya Nghambi wilayani Mpwapwa
Muonekano wa barabara ya Nghambi iliyopo wilayani Mpwapwa.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge akikagua ujenzi wa daraja la Chinyasungwi ambapo amemuagiza Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Salome Kabunda kutomlipa mkandarasi Musons Engineering fedha hadi arekebishe ukuta alioujenga katika daraja hilo.
Muonekano wa daraja la Chinyasungwi lililopo wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge akimuagiza Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Salome Kabunda (hayupo pichani) kutomlipa Mkandarasi Musons Engineering fedha hadi arekebishe ukuta alioujenga katika la Chinyasungwi.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge akiendelea na ukaguzi wa maeneo ya barabara iliyoathiriwa na mvua akiwa eneo la Iyoma lililopo wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Muonekano wa barabara ya Iyoma inayotengenezwa baada ya kuathiriwa na Mvua iliyopo wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge akizungumza mara baada ya kufanya ziara ya kukagua maeneo ya barabara yaliyoathiriwa na Mvua wilayani Mpwapwa.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Jabir Shekimweri,akisisitiza jambo kwa wakandarasi wanaojenga maeneo ya barabara yaliyoathiriwa na Mvua mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge kufanya ziara ya kukagua maeneo hayo.
Kaimu Meneja wa TANROADS Mhandisi Salome Kabunda,akizungumzia ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge ambapo ameagizwa kutomlipa Mkandarasi Musons Engineering fedha hadi arekebishe ukuta alioujenga katika la Chinyasungwi.
Mkandarasi anayejenga kipande cha barabara ya Iyoma Komu Viviani akizungumza mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge kufanya ziara ya kukagua maeneo yaliyoathiriwa na Mvua wilayani Mpwapwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa Bw.George Fuime akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge ambaye amefanya ziara ya kukagua maeneo yaliyoathiriwa na Mvua wilayani Mpwapwa.
Katibu wa CCM Mpwapwa Sophia Kiwanga akimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge kwa kufanya ziara ya kukagua maeneo yaliyoathiriwa na Mvua wilayani Mpwapwa.
…………………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Mpwapwa
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge amefanya ziara wilayani Mpwapwa ya kukagua maeneo ya barabara iliyoathiriwa na mvua ambapo serikali imetenga fedha na kuanza ukarabati wa miundombinu hiyo.
Maeneo hayo ni barabara ya Pandambili-Mlali-Mpwapwa hadi Nghambi,daraja la Chinyasungwi na eneo la Iyoma ambapo zaidi ya Sh Bilioni 2.5 zimetengwa kwa ajili ya kazi hizo.
Akizungumza mara baada ya kukamilisha ziara yake,Dkt Mahenge amemuagiza Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Salome Kabunda kutomlipa mkandarasi Musons Engineering fedha hadi arekebishe ukuta alioujenga wa daraja la Chinyasungwi ambao umepinda.
“Mkandarasi huyu anatakiwa alipwe Sh Bilioni 1.109 lakini nikiangalia hapa naona kabisa ukuta mmoja wa ukingo wa daraja umepinda lakini pia upana wa ukuta huo naona ni mwembamba ilhali eneo hili linapita maji mengi,nikuelekeze Meneja usimlipe mkandarasi fedha hadi arekebishe,”amesisitiza Dk.Mahenge
Sambamba na hilo Dk.Mahenge amesisitiza uwepo wa usimamizi katika maeneo yote ambayo ujenzi unaendelea ili makosa kama hayo na mengine yasiweze kujirudia.
“Kama ukuta unatakiwa kujengwa kwa centimeter 30 ukipunguza hata centimeter 2 unaongelea kupunguza saruji,mchanga na ukipiga hesabu unaona kabisa fedha nyingi zinakuwa zimepotea,hivyo ni muhimu kuhakikisha kunakuwa na usimamizi wa karibu wakati wote,,”alisisitiza Dkt Mahenge.
Aidha Dk.Mahenge amemuagiza Mkurugenzi wa Bahati Investment anayejenga barabara kipande Cha Iyoma kuongeza vitendea kazi na kufanya kazi usiku na mchana ili mvua ikitokea isiweze kuathiri kazi inayoendelea .
Awali Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Jabir Shekimweri ameishukuru serikali kwa kupeleka fedha na kuwezesha ujenzi katika maeneo hayo kuendelea kufanyika na hivyo kuboresha miundombinu iliyopo.
“Eneo hili la daraja la Chinyasungwi yanapita Maji mengi mengine kutoka Mkoani Manyara na katika mvua iliyonyesha mwaka jana kuna kitongoji kilikuwa kisiwa,familia 22 zilikwama huko ikabidi tutafute boti kwa ajili ya kuwatoa,hivyo uwepo wa daraja hili utasaidia Sana kupunguza changamoto hiyo,”amesema Shekimweri.
Hata hivyo Shekimweri amesema kuwa suala la kuimarishwa kwa usimamizi katika maeneo yote yanayoendelea na ujenzi ili kazi inayofanyika iendane na thamani ya fedha iliyotolewa na serikali.
“Kila mmoja wetu awe mzalendo,aumie kuona kazi inayotarajiwa haikamiliki na kuwa katika kiwango bora, tuimarishe usimamizi,tutunze mazingira Ili kuzuia wingi wa maji yanayokuja hapa na katika hili niombe tu kwenye vikao vyetu vile vya kata ajenda ya utunzaji wa mazingira iwe miongoni mwa mambo yanayojadiliwa katika vikao hivyo,”amesisitiza
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TANROADS Mhandisi Salome Kabunda amesema kuwa mipango ya muda mfupi ni kuhakikisha wanakarabati barabara hiyo ili iweze kupitika katika kipindi hiki ambacho wanasubiri mipango ya muda mrefu ya kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
“Hapa tunaendelea na ukarabati ili barabara hizi ziweze kupitika,lakini kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM ilivyoahidi kujenga kwa kiwango cha lami kazi hiyo tutaitekeleza,”amesema Mhandisi Kabunda