**********************************************************
Na Munir Shemweta, WANMM MTWARA
Ujenzi wa Mradi wa Hospitali ya Rufaa Mtwara unaogharimu Bilioni 16 umemvutia Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kulipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kazi nzuri ya ujenzi wa mradi huo utakaohudumia wananchi wa mikoa ya Kusini na nchi jirani.
Akiwa katika siku yake ya kwanza ya ziara yake katika mikoa ya Mtwara na Lindi tarehe 4 Januari 2021, Dkt Mabula alisema pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuwa na changamoto ya fedha lakini liliamua kutumia fedha zake takriban bilioni 2.4 ili kuharakisha ujenzi huo wakati likisubiri malipo yake ya bilioni 2.7.
Naibu Waziri Mabula alisema, uamuzi wa Shirika la Nyumba la Taifa kutumia fedha zake una lengo la kuhakikisha mradi hausimami na wakati huo kuharakisha ujenzi wa mradi huo ili uweze kukamilika na hivyo kuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma pamoja na nchi jirani.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula,Hospitali hiyo ya rufaa mkoa wa Mtwara pamoja na kutumika kwa huduma za kitabibu na mafunzo lakini eneo la hospitali hiyo linaweza kutumika kama sehemu ya utalii kutokana na kujengwa katika eneo la ufukweni mwa bahari ya hindi na kuitaka idara ya ardhi katika halmashauri ya Mikindani kuhakikisha eneo hilo linapangwa katika sura ya kitalii.
” Eneo hili ilipojengwa hospitali ni zuri na linaweza kutumika pia katika utalii naiagiza idara ya ardhi kuweka mpango wa eneo hili utakaoendana na shughuli za utalii kwani kuna fursa inayoweza kumfanya mgonjwa kupata nafuu ” alisema Dkt Mabula.
Naye Mbunge wa Jimbo la Nanyamba mkoa wa Mtwara Dadi Hamis Chikota aliishukuru serikali kwa usimamizi na ufuatiliaji wa ujenzi wa hospitali hiyo na kulipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kasi ya ujenzi na umakini wa hali ya juu unaofanya jengo hilo kuwa na ubora na kuongeza kuwa wabunge wa mkoa wa Mtwara watafuatilia changamoto za fedha ili zipatikane kwa awamu zote kwa lengo la kuwawezesha wananchi wa mikoa ya Kusini kupata huduma za afya ikiwemo za kibingwa.
Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mtwara awali ulitarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2020 lakini sasa uko katika hatua nzuri na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Januari 2021.