Home Michezo LIGI YA NETIBOLI TAIFA YATIMUA VUMBI MANYARA

LIGI YA NETIBOLI TAIFA YATIMUA VUMBI MANYARA

0

********************************************************

Na Mwandishi wetu, Manyara

LIGI ya Taifa ya mpira wa pete (Netiboli) inayoshirikisha mikoa 10 ya Tanzania Bara na Visiwani imeanza kutimua vumbi kwenye uwanja wa Kwaraa Mjini Babati Mkoani Manyara.

Mkurugenzi msaidizi wa maendeleo ya michezo Addo Komba akizindua michezo hiyo Desemba 3 kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema timu zilizoshiriki zinapaswa kuandaa timu za vijana wadogo ili kukuza vipaji.

Komba amesema timu hizo zikianza kukuza vipaji itakuwa maendeleo mazuri kwa mpira wa pete hapa nchini kuanzia ngazi ya vilabu hadi timu za mikoa mbalimbali.

“Pamoja na hayo nitafikisha salamu zenu na changamoto zenu kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa ambaye ni mgeni wizarani,” amesema Komba.

Mwenyekiti wa Chaneta Taifa, Dk Devota Marwa ameupongeza uongozi wa mkoa wa Manyara kwa kufanikisha mashindano hayo kwani mikoa mingine ilisuasua kuandaa.

Dk Marwa amesema baadhi ya mikoa iliyokuwa na nia ya kuandaa michuano hiyo ilishindwa kuandaa kwa kutokuwa na fedha za kugharamikia.

Makamu Mwenyekiti wa chama cha mpira wa pete Chaneta Taifa Anna Gidarya amesema timu 10 zimeshiriki ligi hiyo.

Gidarya ametaja mikoa hiyo ni Manyara, Arusha, Mara, Simiyu, Tabora, Mbeya, Mwanza, Ubungo, Dodoma na Mjini Magharibi ya Zanzibar.

Katika mchezo wa ufunguzi timu ya mkoa wa Manyara ilikuwa inapepetana na timu ya mkoa wa Arusha, kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati.

Ofisa michezo wa mkoa wa Manyara, Charles Maguzu amesema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Abdulrahamani Kololi na baadhi ya madiwani wamejitolea kuchangia gharama za mashindano hayo.