**************************************************
Na Englibert Kayombo – WAMJW, SONGWE
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel amewataka wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika hospitali kutengeneza mfumo wa ufutaliji wa dawa hospitalini ili kuwa na kanzidata ya matumizi sahihi ya dawa.
Dkt. Mollel ametoa agizo hilo alipokutana na Wataalam kutoka Kurugenzi ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi a ya Rais Tawala za Mikoa na Serkiali za Mitaa (TAMISEMI) na timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Songwe kwenye kikao kazi kilichofanyika katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi.
“Kila dawa inayokuja mtutengenezee mfumo ambao tunaona dawa kutoka taifa, unaiona inaingia mkoani, Hospitali ya Wilaya, vituo vya vyote na tuone ni aina gani ya dawa imeingia” Amesema Dkt. Mollel
Dkt. Mollel amesema inawezekana kutengenezwa mfumo rahisi kwa kutumia programu ya ‘Excel’ kwa wataalam hao wakawa na taarifa sahihi ya dawa inayoonyesha matumizi ya dawa toka walivyopokea.
Amesema mfumo huo utawasaidia kutambua mgawanyo wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuwasaidia viongozi kuwa na taarifa sahihi wakati wanashughulikia malalamiko ya uhaba wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya hivyo kuwasaidia katika kufanya maamuzi.
Aidha Dkt. Mollel amewataka wataalam wa afya nchini kuboresha taarifa za takwimu ziwe za ukweli ili kuwasaidia viongozi kufanya maamuzi sahihi kulingana na mahitaji.
“Mnafeli kwenye kufanya maamuzi na wakati mwingine tunaona hamjafanya maamuzi ya busara kumbe mmejifelisha kwa sababu mnashindwa kupata takwimu halisi za magonjwa, idadi ya wagonjwa na mahitaji ya dawa” Amefafanua Dkt. Mollel
Amesema kushindwa kwa wataalam hao kuwa na takwimu sahihi zinasababisha kuwa na mahitaji yasiyo na uhalisia upatikanaji wa dawa.
“Unapoamua kuagiza dawa ni lazima uwe na takwimu sahihi kuanzia taarifa za wagonjwa wa nje hadi wagonjwa waliolazwa, tukiweza kuboresha takwimu zikawa vizuri, tutaweza kuagiza dawa kwa busara na kuhakikisha rasilimali ambazo serikali inatuletea zinatumika kwa busara” amesema Dkt. Mollel