************************************
Na Muhidin Amri,
Nyasa
MKUU wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Isabela Chilumba, amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbambabay hadi wilaya ya Mbinga inayojengwa na kampuni ya Chico kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 103.
Akizungumza baada ya kujionea kazi ya ujenzi katika eneo la mzunguko, Mkuu wa wilaya ameridhishwa na ujenzi wa barabara hiyo ambayo imejengwa kwa ubora wa hali ya juu kusisitiza kuwa, barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Nyasa na Watanzania kwa jumla.
Amesema, kukamilika kwa barabara kutasaidia sana wananchi wa Nyasa kusukuma maendeleo na kumaliza kero ya kusafiri muda mrefu kutoka Nyasa kwenda maeneo mengine ya mkoa wa Ruvuma.
Alisema, awali ilikuwa shida kwa wananchi na magari hasa makubwa yanayotakiwa kupeleka bidhaa mbalimbali kushindwa kufika Nyasa kutokana na miundombinu mibovu,lakini sasa wafanya biashara wa mazao na bidhaa nyingine watafika wilayani humo kwa urahisi.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya, baada ya Serikali kukamilisha ujenzi huo,jukumu kubwa iliyobaki ni wananchi kujipanga na kufanya kazi kwa bidii kwani hawana sababu tena ya kulilia, badala yake waitumie barabara ya lami kama daraja la kujiletea maendeleo.
Aidha, ameishukuru serikali kwa uamuzi wake kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na wao kama serikalii ya wilaya watahakikisha wanailinda na amewataka wananchi kuiona barabara hiyo kuwa yao, hivyo wanapaswa kuwa walinzi wa miundombinu yake.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Kosmas Nshenye alisema, barabara hiyo ina manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii kwani wananchi wa Mbinga kwa sasa wana uhakika wa kusafirisha mazao yao kutoka shambani kwenda sokoni na kusafiri kwenda maeneo mengine kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Alisema, sasa barabara itaanza kutumika kwa ajili ya matumizi ya rasilimali ambazo hapo mwanzoni hazikutumika vizuri kutokana na ubovu wa barabara na kutolea mfano makaa ya mawe yanayochimbwa katika wilaya ya Nyasa ambayo yalishindwa kusafirishwa kwenda viwandani kutokana na ubovu wa miundombinu.
Nhenye,ameiomba jamii kutumia barabara hiyo kama fursa ya maendeleo na kuwataka wananchi wa Mbinga kutumia barabara hiyo vizuri na kuepuka hujumu zozote ambazo zitapelekea kuharibika mapema.
Alisema, barabara ya Mbinga- Mbambabay yenye urefu wa km 66, km 50 iko upande wa wilaya ya Mbinga kwa hiyo ni lazima wananchi wa Mbinga wajivunie kuwepo kwa barabara hiyo ambayo inatajwa kuwa na mchango mkubwa wa kiuchumi.
Gaudence Ndomba mkazi wa Mbinga mjini alisema, barabara hiyo ina manufaa makubwa kwa wananchi wa Mbinga kwani itawezesha wananchi hususani wakulima kusafirisha mazao yao kutoka shambani kwenda kwa walaji.
Ndomba alisema, pia itaboresha baadhi ya huduma muhimu za kijamii kati ya wananchi wa wilaya ya Mbinga,Nyasa na mkoa mzima wa Ruvuma na kuipongeza kampuni ya Chico kwa kukamilisha ujenzi kwa muda muafaka.
Dereva wa basi la kampuni ya Furaha Safari linalofanya safari kati ya Mbinga-Mbambabay-Lundo Erasto Mbepera amefurahishwa na kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo ambapo alisema, awali walilazimika kutumia kati ya masaa 12 hadi 16 kusafiri kati ya Nyasa kwenda Mbinga lakini sasa wanatumia saa 1 tu.
Hata hivyo,amewaomba watu wenye uwezo kuongeza magari ambayo yatafanya kazi ya kusafirisha abiria kwani hakuna kipingamizi kutokana na kukamilika kwa barabara hiyo tofauti na hapo awali.