Na mwandishi wetu, JNHPP
WAZEE ni hazina ya Taifa na kuna msemo wa Kiswahili usemao “Uzee
ni Dawa”, Januari 2, 2021 Wazee Wastaafu
kutoka Chama cha Saidia Wazee Tanzania (SAWATA) walipata fursa ya kutembelea
mradi mkubwa wa kimkakati wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP 2115) unaotekelezwa
kwenye bonde la mto Rufiji na kutoa neno “Vijana mlioko hapa muwe waadilifu”.
Kilichopelekea kutolewa kwa neno hilo ni jinsi wazee hao
walivyostaajabishwa na jinsi ujenzi wa bwawa hilo unavyotekelezwa kisasa tena
asilimia zaidi ya 90 ni vijana wa Kitanzania ndio wametawala eneo hilo la kazi.
“Tumefurahi kuwa
sehemu ya mradi huu, kwa sababu hiki ni chanzo kikubwa cha kuelimisha watoto
wetu, tumeona local content, watanzania wanaoshiriki katika ujenzi wa mradi huu
ni wengi kwa hiyo capacity building inafanyika ipasavyo naomba tuendelee
mujenga uchumi wetu na tuendelee kuijenga nchi yetu.” Alisema Balozi mstaafu
Nyasugara Kadege ambaye alikuwa ni miongoni mwa wazee hao waliotembelea eneo
hilo la Mradi.
Alisema, wameelezwa faida nyingi zitokanazo na mradi huu
ukiacha uzalishaji wa umeme lakini pia Mradi utadhibiti mafuriko ya mara kwa
mara katika maeneo yanayozunguka mto Rufiji na pia utakuza kilimo na uvuvi.
“Nadhani mradi huu utabadilisha maisha ya Watanzania,
kwakweli tunajivunia mradi huu na tunaisifu Serikali na Tanesco kwa kusimamia
mradi huu.” Alisisitiza Balozi Kadege.
Naye mlezi wa SAWATA, Brigedia Jenerali Mstaafu Francis
Xavery Mbena ameipongeza serikali ya awamu ya Tano chini ya uongozi wake Rais
Dkt. John Pombe Masgufuli kwa kutekeleza mradi mkubwa kama huu ambao utaleta
maendeleo makubwa katika taifa letu.
“Tuliomba Serikalini tuje kutembelea bwaha hili la Mwalimu
Nyerere ili tujifunze na kuona utaalamu wa kisasa, kitu cha kushangaza kazi hii
yote nzuri imechangiwa kwa kiasi kikubwa na vijana wetu wa Kitanzania, ninachosema
ni kwamba ingawa wazo la Mradi huu Mwalimu Nyerere alikuwa nalo toka zamani
lakini ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuutekeleza mradi.” Alisema
Jenerali (Mstaafu) Mbena.
Brigedia Jenerali (Mstaafu) Mbena aliwabeza watu wanaokejeli
mradi huo na kuwaita kuwa wana mawazo ya kikoloni. “Mawazo ya Kikoloni yalikuwa kwamba Waafrika
hawawezi kufanya hili au lile lakini ukweli unabaki palepale kuwa kazi hii kwa
sehemu kubwa inafanywa na watu weusi w”enyewe wana uwezo wa kufanya kazi hii na
tuna uwezo wa kupiga hatua katika maendeleo kama ilivyo nchi nyingine.”
Alisema.
Mzee mwingine mstaafu ni Cypriana William ambaye yeye
alisema…“Tulikuwa na hamu ya kuona mradi
huu, tulikuwa tunaona picha tu, lakini baada ya kufika hapa kwakweli nimeona
maajabu, ninampongeza sana Rais wetu kwa kazi hii nzuri na nchi yeyu inastahili
sifa, tumejifunza mengi na tunamuombea Rais baraka tele kwa Mwenyezimungu.”
Alisema mzee huyo mstaafu.
Kwa upande wake
Msimamizi wa Ujenzi wa JNHPP, Mhandisi Said
Kimbanga alisema Tanesco ikishirikiana na Mhandisi kutoka Tanroad watahakikisha
mradi unakamilika kama ulivyopangwa.
“Tumefikia kwenye
hatua nzuri ya kuleta matumaini na wazee leo wameshuhudia kwamba kodi yao
inatumika kutekeleza mradi huu na siyo pesa ya nje, na hadi sasa mradi kwa ujumla
wake umefikia asilimia 40, na ni matumaini yetu ifikapo Juni 22, 2022 mradi
unakamilika.” Alisema Mhandisi Kimbanga.
Mlezi wa SAWATA, Brigedia Jenerali Mstaafu Francis Xavery Mbena na wazee wenzake wakiangalia maajabu….