Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Busolwa, Bw. Baraka Ezekiel, alipotembelea mgodi huo uliopo Kijiji cha Buhunda, Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza, tarehe 30 Desemba, 2020. Kushoto kwa Waziri ni Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Stephen Byabato.
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Busolwa , Bw. Baraka Ezekiel, alipotembelea Mradi wa Mgodi wa dhahabu wa Busolwa tarehe 30 Desemba, 2020. Kushoto kwa Waziri ni Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato.
*************************************************
Na Dorina Makaya,
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kupeleka transfoma mbili zenye uwezo wa MVA 2.5 na MVA 2.0 kwenye mgodi wa dhahabu unaomilikiwa kwa ushirikiano wa kampuni ya Busolwa Mining na Isinka ifikapo tarehe 15 Januari 2021.
Waziri Kalemani ametoa agizo hilo tarehe 30 Desemba 2020 alipotembelea mgodi huo uliopo Kijiji cha Buhunda, Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza.
Waziri Kalemani amesema kuwa, kupatikana kwa transfoma hizo kutawezesha kupatikana umeme wa kutosha kuendesha mitambo mgodini hapo na kupunguza zaidi ya asilimia 70 ya gharama za uzalishaji mgodini hapo.
“ Natambua kuwa tayari mgodi huu uliletewa transfoma kwa ajili ya shughuli za ujenzi lakini ina uwezo mdogo kulingana na mahitaji na transfoma hizi kubwa mbili zilipaswa kuwa zimefika mgodini hapa mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu, na ndio maana nimefika hapa ili kujionea hali halisi na kutoa maelekezo.” Amesema Dkt.Kalemani
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Busolwa Mining Limited, Bw.Baraka Ezekiel alisema kuwa mradi huo ukikamilika, unatarajia kutoa ajira za kudumu kwa watanzania zaidi ya 300 wenye taaluma mbalimbali na utakuwa chachu ya maendeleo kwa maeneo yanayozunguka mgodi wilayani Misungwi, katika mkoa wa Mwanza na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza kufuatia maelekezo ya Waziri Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato, amewataka watumishi wa Mgodi huo kufanya kazi kwa kasi ili kuhakikisha Mradi huo unakamilika kwa wakati na amewasisitiza TANESCO kuhakikisha wanatekeleza agizo la Waziri wa Nishati kama ilivyoelekezwa.