Mbunge wa Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara, mhandisi Samwel Hhayuma akizungumza na wananchi wa eneo hilo kwenye sherehe na ibada ya kumshukuru Mungu kwa kuchaguliwa na wananchi wa eneo hilo kwa kumpa kura nyingi za ndiyo na kushika nafasi hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara mhandisi Samwel Hhayuma (wapili kulia) akiwa na viongozi wa dini na viongozi wa Serikali kwenye sherehe na ibada ya kumshukuru Mungu kwa kuchaguliwa kushika nafasi hiyo.
**********************************
Na Mwanashi wetu, Hanang’
MGUNGE wa Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara, mhandisi Samwel Hhayuma amewatoa asante kwa wananchi wake na kumshukuru Mungu kwa kuchaguliwa kushika nafasi na kudai kwamba atahakikisha anashirikiana na Serikali kuanzisha viwanda ili kuchakata mazao ya mashamba na mifugo ili kuongeza uchumi na ajira kwa wananchi wa eneo hilo.
Mhandisi Hhayuma aliyasema hayo mji mdogo wa Katesh, kwenye sherehe hiyo na ibada ya kumshukuru Mungu na kuwapa asante wananchi wa eneo hilo kwa kumchagua kushika nafasi hiyo.
Amewataka wananchi hao kuunga mkono juhudi za serikali za kuleta maendeleo kwa kufanya kazi kwa bidii kila mmoja katika eneo lake na kuomba ushirikiano katika juhudi zake za Kutaka kuboresha mifugo, kilimo na kufanikisha uanzishwaji wa viwanda.
Amesema kwa kushirikiana na serikali ahadi yake ya kutengeneza kiwanda cha kuchakata nyama ya ngo’mbe katika wilaya hiyo itafanikiwa kwenye kipindi cha uongozi wake.
Amesema ibada hiyo ni njia mojawapo ya kuchota baraka kutoka kwa wananchi wake, wazee na viongozi wa dini lakini pia ni fursa ya kipekee ya kuwaunganisha wananchi wake ili waweze kutafuta kwa pamoja maendeleo ya wilaya hiyo.
Amesema baada ya kushukuru maana yake unafungua milango mipya ya baraka waendelee kuomba mafanikio wanaoenda shambani waombe mvua ili mazao yaliyopo mashambani yasikauke , wafugaji, wafanyakazi wa ofisini wawe na desturi ya kuomba na mafanikio ya Hanang’ ni yetu sote hivyo washirikiane kwa pamoja kuleta mafanikio.
“Tuendelee kumwombea Rais wetu John Magufuli, viongozi wetu wa kitaifa, viongozi wa mkoa, wilaya, kata na vijiji ili waweze kufanya kazi ya kuwatumikia watanzania kwa ufanisi,” amesema mhandisi Hhayuma
Paroko wa parokia ya Endasaki Padri Augustino Hhando amesema hakuna mafanikio yeyote yatakayopatikana bila kumshirikisha Mungu hivyo waendelee kushirikana na kuiombea safari yake ya kuwatumikia wananchi iwe ya haki na aongoze kwa hekima.
“Yeye kama kiongozi wa wananchi ametukumbusha sote umuhimu wa kumshukuru Mungu, hivyo sote tuwe na desturi ya kumshirikisha Mungu katika kila jambo kwani tunaposali tunajiepusha na hila za muovu shetani,” amesema Padri Hhando.
Sheikh wa Wilaya hiyo Ibrahim Athuman amesema mbunge huyo ameonyesha hekima yake ya kujali wananchi wake wote bila kujali dini zao itikadi na makabila hivyo aliwataka wananchi kuendelea kumwombea katika utekelezaji wake wakiwa katika nyumba zao za ibada.