Mwenyekiti wa Bodi ya Shule sekondari Muzimuni Bw.Alpherio Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ujenzi wa madarasa katika shule hiyo magomeni Jijini Dar es Salaam.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa madarasa
***************************************************
NA EMMANUEL MBATILO
Katika kutekeleza agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu, Uongozi wa bodi ya Shule ya Sekondari Muzimuni iliyopo Magomeni Jijini Dar es Salaam wanaendelea na ukamilishaji wa madarasa ya vyumba sita katika shule hiyo ili shule zitakapofunguliwa yawe yamekamilika.
Akizungumza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo Bw.Alpherio Nchimbi amesema wao kama viongozi wanaofuatilia ujenzi huo wameridhika na kasi ya ujenzi huo na wana uhakika mpaka shule zitakapofunguliwa ujenzi utakuwa umekamilika kwa kiasi kikubwa.
“Kazi inaendelea vizuri hii kazi ni ya siku ya tatu mpaka sasa na muda uliobaki utatosha kwa maana kazi hapa inafanyika usiku na mchana”. Amesema Bw.Nchimbi.
Amesema wanamshukuru Rais Dkt.John Pombe Magufuli pamoja na Wizara husika kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha ujenzi wa madarasa unakamilika kwa wakati.
Kwa upande wake mmoja wa mafundi katika shule hiyo Justin Ngube amesema wao wataendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha ujenzi huo unamalizika kwa wakati ili kupisha masomo kuendelea shule zitakapofunguliwa.