*******************************************
Mbunge wa Makete, Festo Sanga ametekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu 2020, ya kufunga umeme jua katika zahanati ya Kijiji cha Ilindiwe, kata ya Mang’oto jimboni humo, kutokana na wananchi kukosa baadhi ya huduma usiku huku wahudumu wa afya wakilazimika kutumia tochi kutoa matibabu.
Akikabidhi umeme huo leo, Mbunge Sanga amesema wakati kuomba kura wananchi hao walimwambia adha wanayoipata ya kukwama kupata huduma nyingine usiku.
“Nilipokuja mliniambia hitaji lenu la kwanza ni Umeme wa Solar kwenye zahanati yenu hii, mlihitaji umeme kwasababu huduma nyingi zinakwama nyakati za usiku na hata zile zinazohitaji umeme. Zahanati hii inategemewa na sehemu kubwa ya wananchi wa Mang’oto, nimeona ni vyema nikaitekeleza mapema ili Mama zetu wanapohitaji huduma ya uzazi waipate masaa yote pakiwa na umeme,”amesema
Amesema hatua hiyo itawaondolea adha wahudumu wa afya ya kutumia tochi kuhudumia wananchi nyakati za usiku.
“Nawaomba mzitunze solar hizi ili zitusaidie kwa muda mrefu wakati tunahangaikia umeme wa REA,”amesema.
Nao, Baadhi ya Wananchi walioshuhudia utekelezaji wa ahadi hiyo wamesema, wameshangazwa na namna Mbunge alivyotekeleza ahadi hiyo kwa uharaka kwasababu ni ahadi ambayo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kwanza wa Mkoa wa Njombe na baadae viongozi wengine lakini haikutekelezeka.
“Huyu Sanga ametupa matumaini makubwa sana sisi wananchi wa Ilindiwe tunamuombea kwa Mungu ambariki kwa pale alipotoa kwaajili yetu,”amesema mmoja wa wananchi.